MKUU WA MKOA WA MARA AZITAKA HALAMASHAURI KUSIMAMIA FEDHA ZA RUZUKU ZA AGPAHI.


Mkuu wa mkoa wa Mara Mhe.Adamu Malima (aliyesimama) akitoa maagizo kwa viongozi wa Mkoa mara baada ya uwasilishwaji wa taarifa mbalimbali za Mkoa huo katika kikao cha kamati ya ushauri ya Mkoa. Kushoto kwake ni DC wa Musoma, Dr.Vicent Naano na kulia kwake ni Kaimu Katibu Tawala Mkoa Josephati Nyanda.

Meneja wa AGPAHI kanda ya Ziwa Dr. Nkingwa Mabelele akiwasilisha taarifa katika kikao cha (RCC).

Sehemu ya viongozi wa ulinzi na usalama wakifatilia kikao cha ushauri cha Mkoa (RCC).

Mkuu wa wilaya ya Tarime, Mh.Glorious Luoga (kushoto) akiwa na mkuu wa wilaya ya Serengeti, Mh.Nurdin Babu (aliyeshika mikono) kwenye kikao hicho.

Viongozi wa dini wakifuatilia kikao.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mara Dr. Francis Mwanisi akiwasilisha taarifa katika kikao cha ushauri ( RCC).
Na makaliblog.Mara
Serikali mkoani Mara imesema itashirikiana na mashirika yasiyokuwa ya kiserikali yanayotekeleza miradi mbali mbali ya maendeleo mkoani humo.

Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa mkoa wa Mara, Mhe. Adam Malima wakati wa kikao cha ushauri wa Mkoa wa Mara (RCC) kilichofanyika katika Manispaa ya Musoma ambapo aliweka wazi kuendelea kushirikiana vyema na shirika la AGPAHI, ambalo hujishughulisha na mapambano ya Virusi vya Ukimwi.

Pia Mhe. Malima aliziagiza Halmashauri zote Mkoani humo kupitia wakurugenzi kuhakikisha kuwa zinatoa ushirikiano wa matumizi bora wa ruzuku zinazotolewa na AGPAHI katika kutekeleza shughuli mbalimbali za miradi ya Ukimwi.

" Simamieni fedha hizi mnaona sisi hapa tunashikana mashati ili kupata shilingi billion 20 kwa ajili ya kukamilisha ukarabati wa Hospitali ya Mwalimu Nyerere, lakini hawa wanatoa fedha za kutosha na kwa wakati, tusiwakatishe tamaa kwa kuchelewa kutuma taarifa ya utekelezaji wa fedha hizo," Malima alisisitiza.

Naye Meneja wa AGPAHI kanda ya Ziwa Dr. Nkingwa Mabelele alisema Shirika la AGPAHI linajishughulisha na miradi ya kutokomeza maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) na Ukimwi, kuzuia maambukizi mapya ya VVU kwa watoto, matunzo na matibabu kwa watu wanaoishi na VVU. Shirika la AGPAHI linatekeleza miradi yake katika mikoa ya Geita, Mara, Mwanza,Shinyanga,Simiyu, Tanga na Manyara.
Katika Mkoa wa Mara, shirika la AGPAHI linatekeleza mradi wa 'Boresha' ambao sasa umeonekana kuwa na manufaa kwa watu wanaoishi na VVU.

Awali akitoa taarifa ya utekelezaji wa miradi huo katika kikao cha RCC, Dr. Mabelele alisema mradi wa Boresha ni wa miaka mitano na ulianza kutekelezwa mwaka 2016 na kutarajiwa kukamilika mwaka 2021.

Aliongeza kuwa fedha za ruzuku zinazotolewa husaidia kuratibu shughuli mbalimbali za Ukimwi ili kuboresha utoaji huduma bora za Afya, kusaidia Halmashauri kufanya usimamizi na ufatiliaji wa utoaji wa huduma za Ukimwi katika maeneo husika.

"Vituo vya afya vimefanikiwa kununua vifaa tiba ikiwemo vifaa vya kuangalia ongezeko la Virusi vya Ukimwi (VVU) kwa watu wanaoishi na VVU," alisema Dr. Mabelele.

Kwa kipindi cha Oktoba 2016 hadi Septemba 2017 Shirika la AGPAHI limeweza kupima VVU watu wapatao 199,889 na kati ya hao 7325 walikutwa na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU).

Mganga mkuu wa Mkoa wa Mara, Dkt.Francis Mwanisi alishauri mkoa wa Mara kuunga mkono juhudi za shirika la AGPAHI kutokana na ushirikiano ulioonyeshwa katika miradi ya Ukimwi kwani wamekuwa sehemu kubwa ya msaada wa huduma ya afya katika vituo vya afya mkoani Mara.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Musoma Dr.Vicent Naano, aliliomba shirika la AGPAHI kuzishirikisha Halmashauri wakati wa upangaji wa ruzuku za miradi kutekelezwa kwani itasaidia kuondoa changamoto ya halmashauri kurudia kutenga fedha katika vituo hivyo.
Kikao cha kamati ya ushauri ya Mkoa (RCC) ni kikao  ambacho kinawakutanisha wadau wa sekta mbalimbali za utekelezaji wa miradi mbalimbali mkoani Mara ambao hukutana mara mbili kwa mwaka kwa lengo la kupokea taarifa za utekelezaji wa miradi.
Powered by Blogger.