Licha ya kupata timu, Agyei bado aililia Simba;



KIPA wa zamani wa Simba, Daniel Agyei amesema anamshukuru Mungu amepata timu nchini Ethiopia lakini bado hajawasahau Wekundu hao wa mtaa wa Msimbazi.
Agyei amesaini mkataba wa mwaka mmoja kuitumikia klabu ya Jimma City iliyopanda daraja msimu huu wa ligi kuu nchini Ethiopia unaotarajiwa kuanza mwishoni mwa mwezi huu.

Akizungumza asubuhi ya leo, Agyei alisema amejipanga kuibeba timu hiyo kama ambavyo alijitoa kwa Simba kabla hajatupiwa virago na nafasi yake kupewa mzawa Aishi Manula.
“Nimesaini mkataba wa mwaka mmoja tu, ila kiukweli naikumbuka sana Simba, mashabiki wake ni watu wazuri siku zote, nakumbuka sana ile kaulimbiu yao ya Nguvu Moja,” alisema Agyei.

Akizungumzia alivyoondoka Simba Agyei alisema alitamani sana kuendelea kuitumikia Simba lakini viongozi walimweleza wazi kuwa hana nafasi tena kikosini hapo.
“Walinitaarifu nikiwa kwetu kuwa hawanihitaji tena kwavile kiwango changu kiko chini, niliumia sana kwavile licha ya kazi lakini nimetokea kuipenda Tanzania, siku wakinihitaji wao au timu yoyote hapo nitarudi,” alieleza Agyei kwa masikitiko makubwa.

Agyei tayari ameshaichezea Jimma mchezo mmoja wa michuano ya City Cup dhidi ya Ethiopia Coffee ambao ulimalizika kwa sare ya bila kufungana.
Powered by Blogger.