NDALICHAKO AITWA GAMBOSHI.........

Mhashamu askofu Liberatus Sangu wa Jimbo la Shinyanga akiongoza maadhimisho ya misa takatifu ya kipaimara ambapo waimarishwa 200 walipewa kipaimara Gamboshi, huku akiwataka viongozi wa serikali kulitazama eneo hilo hasa kupeleka elimu ili kuibadili jamii hiyo iliyokuwa inasifika kwa ushirikina.

Askofu Liberatus Sangu akiwapa kipaimara waumini wa kanisa hilo la Gamboshi ili kuwaimarisha kiroho.


Wanakwaya wa Parokia ya Ngulyati wakiimba kwenye maadhimisho ya misa hiyo Gamboshi juzi jumatano,

Diwani wa kata ya Gamboshi Bahame Kaliwa akiongesa na waumini na wananchi waliohudhuria katika adhimisho la misa hiyo juzi, na kusema kuwa eneo hilo ni salama, lakini linakabiliwa na uhaba wa miundombinu ya elimu.
WANANCHI wa Kata ya Gamboshi wilayani Bariadi mkoani Simiyu wamemwomba waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako kufika katika kijiji hicho ili kutatua changamoto za kielimu zinazolikabili kijiji hicho. na kulifanya kuwa nyuma kimaendeleo.
Mbali na Waziri huyo, Viongozi wengine ambao wamekuwa wakiogopa kufika eneo hilo kutokana na historia yake kuwa ni kijiji cha wachawi wameombwa kufika na kutatua changamoto hizo ili kuifuta dhana iliyokuwa imejengeka kuwa ni ki jiji cha wachawi.
Akiwasilisha maoni hayo ya wananchi kwenye misa ya kipaimara iliyoadhimishwa kijijini hapo, Diwani wa kata hiyo Bahame Kaliwa amemtaka waziri huyo kufika ili kujionea changamoto za kielimu hasa wingi wa wanafunzi madarasani na pia ajionee miundombinu duni ambayo hawawezi kuimaliza kwa haraka.
‘’hii dhana ya ushirikina iliyokuwa imejengeka haiwezi kuondolewa bila elimu…hivyo tunamwomba waziri wa elimu tunamwomba afike hapa aje aone watoto walivyowengi, na aone miundombinu ilivyoduni ambayo haiwezi kuondolewa kwa uharaka, hasa neon lililojengeka la ushirikina’’ alisema Kaliwa.
Kwa upande wake Askofu wa Jimbo la Shinyanga Mhashamu Liberatus Sangu amewataka viongozi wa serikali kuyafikia maeneo ambayo yalikuwa yamesahaulika ikiwemo Gamgoshi, na kuyapelekea miundombinu na kuwafungua watu hao ili waweze kubadilika kifikra, kimaono na kimtazamo.’
Sangu aliongeza kuwa ikiwezekana wanafunzi wote waliohitimu elimu ya msingi kijijini hapo wawe wamefaulu au hawajafaulu waende sekondari ili baada ya kuhitimu waweze kuibadilisha jamii ya eneo hilo, na kuwafungua wapate elimu.
‘’viongozi wa ngazi za serikali waje kuyafikia maeneo hayo…wanafunzi wote waliohitimu darasa la saba waende wote sekondari hata kama hawajafaulu ili kuibadili jamii yao iweze kuondokana na ukatili wa mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi kwa sababu wote wamezaliwa na kuumbwa kwa sura na mfano wa mungu’’ alisema Sangu.
Nao baadhi ya wananchi waliohudhuria Maadhimisho ya misa hiyo takatifu ya kipaimara walisema kuwa eneo hilo kwa sasa ni tulivu tofauti na inavyoaminika kwa sababu ni sawa na maeneno mengine ya nchi na watu wanaoishi huku ni wa kawaida sana, alisema Danieli Mvungi kutoka Morogoro aliyekuwa amehudhuria misa hiyo.
Padri wa parokia ya Ngulyati John Nkinga alisema kuwa hadi sasa kuna mabadiliko makubwa kutokana na watu wa eneo hilo wameanza kubadilika kiimani kwa kumcha mungu, ambapo jumla ya waimarishwa 200 walipewa kipaimara katika kanisa la Mtakatifu Petro Gamboshi.