YANGA WAUNGANA NA SIMBA KUWAOMBEA, AVEVA NA KABURU;


UONGOZI wa klabu ya Yanga umesema upo pamoja na watani wao wa jadi Simba kwenye kipindi hiki kigumu kufuatia viongozi wake wakuu kushikiliwa na vyombo vya dola kutokana na tuhuma za kughushi nyaraka za klabu na utakatishaji fedha.

Rais wa Simba Evans Aveva na Makamu wake Geofrey Nyange ‘Kaburu’ wanashikiliwa na jana walipandishwa kizimbani katika Mahakamana ya Hakimu Mkazi Kisutu, kesi yao ilipotajwa kwa mara ya pili na kutokana na kesi hiyo kutokuwa na dhamana watuhumiwa walirudishwa rumande hadi Julai 20.

Katibu mkuu wa Yanga Boniface Mkwasa alisema wanajua viongozi na wanachama wa klabu ya Simba wanapitia katika kipindi kigumu ila wanaungana nao kwakuwa na wao iliwahi kuwatokea kwa Mwenyekiti wao Yusuph Manji.


“Nafahamu watani wetu Simba wapo katika kipindi kigumu kufuatia matatizo ya viongozi wao wakuu, sisi pia iliwahi kututokea. Kwa niaba ya uongozi wa Yanga tunawaombea wenzetu kheri wamalize salama jambo hilo,” alisema Mkwasa.

Katika hatua nyingine Mkwasa alisema kesho Jumamosi Makamu Mwenyekiti Clement Sanga atakutana na wachezaji wa zamani wa mabingwa hao kwa ajili ya kuwaenzi kutokana na mchango wao mkubwa walioutoa kwa klabu hiyo.


“Makamu Mwenyekiti atakutana na wachezaji wa zamani wa Yanga kesho kujadili masuala mbalimbali ikiwemo kuwaenzi kutokana na mchango wao mkubwa kwa klabu,” alisema Mkwasa.

Tayari kikosi cha timu ya Yanga kimeanza mazoezi kwa ajili ya kujiandaa na msimu mpya wa ligi utakaoanza Agosti 26 mwaka huu.
Powered by Blogger.