YANGA NUSU MORO, NUSU MBEYA;
KIKOSI cha timu ya Yanga kimeondoka mchana wa leo kuelekea mkoani Morogoro kwa ajili ya kambi huku wadogo zao wa Yanga B wakiondoka asubuhi kwenda jijini Mbeya kwa ajili ya mechi ya kirafiki dhidi ya Mbeya City kesho kwenye uwanja wa Sokoine.
Kikosi kilichoenda Mbeya chini ya kocha msaidizi Shadrack Nsajigwa kitashuka dimbani kesho kucheza dhidi ya City katika mchezo ulioandaliwa na tume ya kudhibiti UKIMWI Tanzania ( TACAIDS).
Mkuu wa Idara ya Habari na mawasiliano wa klabu ya Yanga, Dismas Ten amesema kuwa kikosi cha timu hiyo kitagawanywa mara mbili wengine wataenda kuweka kambi Morogoro kwa ajili ya maandalizi ya ligi kuu ambacho kitaondoka mchana, huku wengine wakiondoka asubuhi kuelekea jijini Mbeya tayari kwa mchezo wa kesho.
“Yanga ni timu kubwa na ina kikosi kipana, ni kweli kesho tutakuwa na mchezo wa kirafiki dhidi ya Mbeya City na timu ipo njiani inaelekea mkoani humo. Wachezaji wengine wataondoka mchana kuelekea Morogoro kwa ajili ya kambi ya maandalizi ya ligi,” alisema Ten.
Kwa upande wake msemaji wa Mbeya City, Shah Mjanja amesema mashindano hayo yatahusisha timu nne ambazo ni pamoja na Simba B na Tanzania Prisons ambazo zitacheza keshokutwa katika uwanja huo.
Shah alisema baada ya mchezo huo timu yao itasafiri kuelekea mkoa Morogoro kucheza mechi ya kirafiki dhidi ya Mtibwa Sugar.
“Baada ya mchezo wetu dhidi ya Yanga kesho, timu itasafiri kuelekea Morogoro kucheza na mechi ya kirafiki dhidi ya Mtibwa,” alisema Shah.
source boiplus