WATU WASIOFAHAMIKA WATEKETEZA KWA MOTO BANDA LA KUKU, WAACHA UJUMBE MZITO;

Jiko la Muuguzi wa zahanati ya Guduwi kama linavyoonekana baada ya kuchomwa moto na watu wasiofahamika usiku na kusababisha kuku zaidi ya 30 kufia humo. (Picha zote na COSTANTINE MATHIAS).


Maandishi ya maneno yaliyoandikwa na watu wasiofahamika yenye ujumbe mzito kulizunguka jengo hilo ambapo hadi sasa hakuna mtu yeyote anayehusishwa na tukio hilo.
Na COSTANTINE MATHIAS, Simiyu.
KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida watu wasiofahamika wamechoma jiko la muuguzi wa zahanati ya Guduwi iliyoko Halmashauri ya mji wa Bariadi mkoani Simiyu huku wakiandika na kuacha ujumbe mziti wenye maneno ya uchochezi yanayohatarisha amani kuzunguka jengo la zahanati hiyo.

Uchunguzi uliofanywa na Makaliblog umebaini kuwepo kwa mgogoro mkubwa katika zahanati hiyo baina ya watumishi, jamii na viongozi wa mitaa hali inayofanya hata zoezi la utoaji wa huduma za afya katka eneo hilo kudorora huku chanzo kikidaiwa kuwa ni kuingizwa kiholela kwa wahudumu wa afya ngazi ya kijiji bila kufuata taratibu na sera za afya.


Inadaiwa kuwa usiku wa kuamkia july 11, mwaka huu watu hao walichoma jiko la muuguzi huyo (jina linahifadhiwa) na kuteketeza kuku zaidi ya 30, mkaa magunia mawili na mabti matano, na baada ya kutekeleza adhima hiyo walikwenda kwenye jengo la zahanati na kuanza kuandika maneno mbalimbli ya kutaka kutimiza uhalifu kuzunguka jengo zima.


Baadhi ya maneno yaliyoandikwa katika jengo hilo kwa lugha ya Kiswahili na kisukuma ni pamoja na ‘’Bagosha nesi jizi twelemano’’ (wanaume nesi mwizi tumekataa), hatumutaki nesi, Nesi mkomba uji, hafai mwomba kuku, kila mzazi 10,000/=, muondoeni msipofanya hivyo tutachoma na jengo hili’’ ambapo hadi sasa yanaonekana kuandika kwa kutumia rangi nyeusi.


Akiongea juu ya tukio hilo Mganga mfawidhi wa zahanati hiyo Leonard Pontian alisema kuwa mahusiano yao na jamii yanaonyesha dhahiri kuwa hawako sawa ndiyo maana wameamua kufikisha ujumbe kwa njia ya maandishi na kuchoma moto.

Baadhi ya wananchi wanaozunguka kituo hicho wanamtupia lawama mganga huyo ambaye ana miezi minne tangu ahamishiwe hapo kuwa amewagawa wahudumu hao huku akiongeza wengine toka mtaani wasiokuwa na taaluma yoyote ya utoaji wa huduma za afya.

‘’kumekuwepo na wahudumu wa afya wengi mno katika zahanati hii tumeshindwa kubaini mhudumu halali na aliyesomea ni yupi…na zahanati hii ikifungwa ni athari kwa jamii na wakitekeleza yaliyoandikwa hapa, wananchi watakuwa wamepoteza nguvukazi na serikali itakuwa na kazi ya ziada ya kujenga upya’’ alisema Shelewe Kishiwa.

Diwani wa kata ya Guduwi Yohana Mnyumba alisema kuwa hajafika eneo la tukio kwa sababu alikuwa na msiba lakini taarifa zote anazo na ameagiza serikali za mitaa (watendaji na wenyeviti) wakae na kujadili juu ya tukio hilo na maadhimio watakayoyafikia nay eye atayaunga mkono.


Kaimu Mwenyekiti wa mtaa wa Guduwi Mbugani Mpanda Mabula alisema kuwa ushirikiano uliopo baina ya jamii na zahanati hiyo ni mdogo sana kutokana na muuguzi na mganga kutoshirikiana na kusababisha utoaji wa huduma za afya kuwa duni.

‘’hadi sasa hakuna mlinzi kutokana na ushirikiano duni baina yetu na zahanati hiyo, kulitokea kutofautiana kuteuwa watoa huduma ngazi ya jamii hivyo hadi sasa hatuwatambui watoa huduma walioko pale’’ alisema Mabula.

Aliongeza kuwa serikali ya mtaa imekaa na kupendekeza watumishi wote wahamishwe ili kunusuru hali hiyo kwa sababu wakiaachwa inaweza leta madhara makubwa ikiwemo kuharibu mali na majengo kama maandishi yanavyosomeka.


Mtendaji wa mtaa huo Fred Joseph alisema kuwa kutekelezwa kwa adhma ya maandishi hayo ni hasara kwa umma na pia migogoro iliyoko pale ni ya watumishi kwa watumishi huku wakiiomba serikali kuingilia kati suala hilo ili kunusuru rasilimali zilizopo.


Aliongeza kuwa tayari wamekaa vikao na wananchi na kupendekeza mmoja wa watumishi hao ahamishwe, ambapo tayari wameshamwandikia mganga mfawidhi wa halmashauri barua za maombi yao na kusubiri utekelezaji na wahudumu wa afya watasimamishwa kazi mara moja.

Mganga Mfawadhi wa Halmashauri ya mji wa Bariadi Akilimali Mpozemenya alisema kuwa jambo hilo liko kwenye vyombo vya ulinzi na usalama hawawezi kuliingilia kuwahamisha watumishi hao hadi pale kamati hiyo itatoa maamuzi.


Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya ambaye ni Mkuu wa wilaya ya Bariadi Festo Kiswaga alisema kuwa wanaendelea na uchunguzi lakini wote walioshiriki kitendo hicho watafikishwa mahakamani kwa kuwa vitendo hivyo ni vya kiuhalifu na uvunjifu wa amani.

‘’kitendo cha kuchoma jiko moto, kuandika maneno ya kiuharifu ni uvunjifu wa amani na uchochezi hivyo wote walioshiriki katika kitendo hicho tuwakamata na kuwapeleka mahakamani, na ukizingatia jengo hilo linatoa huduma ya kitabibu kwa wananchi hatutakubali vitendo hivyo kuendelea’’ alisisitiza Kiswaga.

                          KWA HABARI NA MATUKIO TUPIGIE KWA 0754295996
                Toa maoni yako matusi    ( hapana)
Powered by Blogger.