Mamia wakamatwa maandamano ya kupinga serikali Urusi
Polisi wa kupambana na fujo nchini Urusi, wamewakamata na
kuwazuilia mamia ya waandamanaji waliokuwa wakipinga madai ya ufisadi
katika Serikali ya nchi hiyo.
Maandamano makubwa mno yameshuhudiwa katika miji ya Moscow
na St Petersburg, mahali ambapo maelfu ya waandamanaji walijitokeza,
huku wengi wao wakipiga kelele kumlaani Rais Vladimir Putin.
Polisi wamemtia mbaroni mwandalizi wa maandamano hayo
Alexei Navalny ambaye ni mkosoaji wa serikali na kiongozi mkuu wa
upinzani nchini Urusi, Kiongozi mkuu wa idara ya usalama nchini Urusi,
alitaja maandamano hayo kama ya uchokozi.
Wengi wa waandamanaji walifoka "Putin is a thief!" yaani "Putin ni mwizi" "Russia will be free" yaani "Urusi itakuwa huru!"
Zaidi ya watu 600 wanadaiwa kukamatwa na kuzuiliwa na
maafisa wa polisi wa kupambana na fujo katika mji mkuu Moscow, na
wengine 300 wamekamatwa katika mji wa St Petersburg.
Bw Navalny anatazamiwa kumpinga Rais wa Vladimir Putin
katika kiti cha Urais kwenye uchaguzi mkuu mwaka ujao, Rais Putin
hajatangaza rasmi iwapo atawania tena kiti hicho au la.