Kada ahama CHADEMA kuungana na JPM baada ya Ripoti ya Makinikia
Siku moja baada ya Rais JPM kupokea Ripoti ya Pili ya Makinikia yenye gumzo Ikulu DSM, mwanasiasa aliyewahi kugombea Ubunge Jimbo la Sengerema 2015 kupitia CHADEMA,Hamis Tabasamu amekihama Chama hicho akidai kimekuwa mstari wa mbele kupinga juhudi za Rais katika kuyakomboa madini nchini.
“…imepokelewa taarifa nyingine ya Pili ya madini lakini mimi kama mtu mzima kwa nafasi yangu na uelewa wangu. Mimi kama kada wa CHADEMA Kanda ya Ziwa nilikuwa Mgombea wa Ubunge katika Jimbo la Sengerema nikapata kura kama 40,000 mwaka 2015.
“Moja ya vitu ambavyo tumezunguka sisi katika maeneo yetu haya yanayochimbwa madini ambayo sisi Sengerema pia ni waathirika pia wa jambo hili, ni kwamba tulilalamikia sana kama Chama uchimbaji wa madini na mikataba hii iliyopo ya hawa wawekezaji wa sekta ya madini.
“Jambo hili lilinifanya mimi nikawa miongoni mwa watu ambao niliingia vitani kupambana kuhakikisha kwamba jambo hili linawekwa sawa na Watnzania wananufaika na madini yao. Ndani ya Chama changu sisi tena ambao tuliozunguka kwa kuruka na Helkopta tukipiga vita, tukiwaaminisha Watanzania hasa wa Kanda ya Ziwa tukiwaeleza kabisa kwamba tunaibiwa, tunaibiwa.
“Leo sisi ndio tumekuwa wa mwanzo kupiga vita jambo hili. Sasa jambo hili limeniumiza sana. Taarifa ya leo imenifanya mimi siwezi kuwa mnafiki lazima niwe Mtanzania mzalendo katika jambo hili. Ni kwamba leo naondoka CHADEMA kwa jambo hili. Naondoka CHADEMA mchana kweupe kama nilivyoingia.
“Niliingia mchana kweupe natoka CCM nikitegemea kwamba CHADEMA kitakuwa ndio Chama kitakachokuwa mkombozi kwa Watanzania lakini leo viongozi wamegeuka kuwa tofauti na jambo hili. Nimesikitika sana.
“Japo Mwenyekiti wetu wa Chama hajazungumzia jambo hili lakini viongozi waandamizi wa CHADEMA wanalizungumzia jambo hili kama kuonesha kwamba Rais Magufuli jambo analolifanya ni baya, ni baya kupita kiasi. Sasa je, kama mheshimiwa Rais Magufuli kama hili jambo asipolifanya leo litakuja kufanywa na nani?” – Hamis Tabasamu.