Wananchi watema cheche, wataka Marais wastaafu wachunguzwe
Mikoani. Wananchi katika maeneo mbalimbali nchini
wamemshauri Rais John Magufuli kufanya mabadiliko ya Katiba na
kuhakikisha diplomasia ya uchumi haivurugiki kutokana na sakata la
mchanga wa madini (makinikia).
Wakitoa maoni yao jana, baadhi ya wananchi walisema licha
ya viongozi walioongoza Wizara ya Nishati na Madini, wanasheria wakuu na
watendaji wengine wa Serikali kutajwa katika ripoti ya kamati ya pili
ya uchunguzi wa makinikia, Katiba ibadilishwe ili iweze kuruhusu marais
wastaafu kuchunguzwa na kushtakiwa.
Maoni kutoka Kanda ya Ziwa
Baadhi ya wananchi kutoka mikoa ya Mara, Geita, Shinyanga,
Mwanza na Kagera pia walipendekeza utaratibu wa kisheria ufanyike
kutaifisha mali za watu binafsi na kampuni zilizohusika na hujuma katika
sekta ya madini.
Mkazi wa mjini Tarime, Abdul Ahmed, alishauri kampuni
zilizobainika kufanya udanganyifu zifilisiwe na watendaji wake
kushtakiwa au kufukuzwa nchini. Pia alipendekeza Katiba na sheria
zibadilishwe kutoa fursa ya uchunguzi wa kijinai dhidi ya marais
wastaafu kubaini iwapo walihusika au walijua na kunyamazia hujuma katika
sekta ya madini.
“Nadhani tubadilishe hili ili kuongeza nidhamu na hofu kwa wanaokabidhiwa dhamana ya uongozi,” alisema Ahmed.
Alisema uwapo wa kifungu cha viongozi wote kuwajibishwa kwa
makosa ya jinai wanayotenda au kunyamazia kwa nafasi zao, kitarejesha
nidhamu ya utumishi.
Wasemavyo Manyara, Arusha
Chama cha Wachimbaji wa Madini Mkoa wa Manyara (Marema) na
mtandao wa mashirika yasiyo ya kiserikali Mkoa wa Arusha (Angonet),
wameunga mkono hatua ya Rais lakini wakamtaka kukutana na mabalozi wa
nchi zinakotoka kampuni zinazochimba madini ili kuzungumzia
yaliyobainishwa na kamati za uchunguzi.
Kwa nyakati tofauti wenyeviti wa Marema, Sakidi Mnenei na
wa Angonet, Petro Ahham walisema Rais ana nia njema katika sakata la
utoroshwaji madini lakini ili kuungwa mkono zaidi, wadau wengine
wanapaswa kuhusishwa.
Mnenei alisema ili kuepuka kuvuruga diplomasia ya kiuchumi
ni vyema sasa Rais Magufuli akakutana na mabalozi wa nchi ambazo kampuni
hizo zinatoka ili kuwapa taarifa na mapendekezo ya Serikali hasa baada
ya kubainika kuwapo wizi.
“Nia ya Rais ni nzuri tumeibiwa kiasi cha kutosha sasa,
tutoke hapa bila kusababisha athari nyingine za kiuchumi na ni vyema
mikataba ya madini ipelekwe bungeni na ipitiwe upya,” alisema.
Ahham alisema vita ambayo Rais anapigana ni kubwa lakini
anapaswa kushirikiana na mashirika yasiyo ya kiserikali (NGO) na asasi
zingine ili kusaidia ushindi.
Mkurugenzi wa Shirika la Haki Madini, Aman Mustapha licha
ya kueleza kuwa anaunga mkono jitihada za Serikali, alisema upotevu wa
fedha ambao unatajwa unaonyesha udhaifu mkubwa serikalini.
Ushauri kutoka Mbeya
“Tunamshukuru Rais kwa uzalendo lakini asiwaonee huruma,
achukue uamuzi wa kuzuia mali zao ndipo hatua ya kuwapeleka mahakamani
ifuatwe,” alisema Aggrey Kandonga ambaye ni muasisi wa Chadema mkoani
Mbeya.
Diwani mstaafu wa Kata ya Itezi jijini Mbeya, Frank Maemba
alisema watumishi wa BoT wanapaswa kuwajibishwa kwa kuwa wao ndio
wanaosimamia uchumi wa nchi.
Source: Mwananchi