WAFUGAJI WAITIKIA UPIGAJI CHAPA MIFUGO.
Na mwandishi wa MAKALIBLOG, S Mifugo ikipigwa chapa.
WAFUGAJI wilayani Maswa mkoani
Simiyu wameitikia agizo la serikali la upigaji chapa na utambuzi wa mifugo yao hali
itakayowaondolewa wizi wa mifugo na kupunguza migogoro baina yao na wakulima.
Aidha Wafugaji hao wamesema kuwa
zoezi hilo litawapunguzia milipuko ya magonjwa kwa kuwa mifugo yao inatambulika
kwa alama na idadi halisi huku wakiowaomba wataalamu wa mifugo kuwafikia mara
kwa mara na kundeleza mahusiano waliyoyaanzisha.
Wakiongea wakati wa upigaji chapa mifugo
katika kijiji cha Mwaliga, kata ya Shishiyu wilayani humo walisema kuwa
wamekubali kwa hiari yao kupigiwa chapa mifugo yao ili kuepusha kuibiwa mifugo,
pia kutambua idadi ya mifugo wao na wafugaji wenyewe kutambulika.
Medardi Msugwa mkazi wa kijiji hicho
alisema kuwa baada ya kupewa elimu na kutambua umhimu wa mifugo kupigwa chapa,
wafugaji wenyewe wanaleta mifugo yao kwa hiari huku wakija na gharaza za
kupigiwa chapa shilingi mia tano kwa kila mfugo.
‘’gharama ya shilingi mia tano kwa
kila mfugo ni kubwa kama una mifugo mingi…hatuna namna inabidi tutoe kulingana
na mahitaji ya serikali ya kuwa kila mfugaji apigiwe chapa mifugo yake ili iweze
kutambulika’’ alisema Kija Msugwa.
Afisa Mifugo wa Wilaya hiyo,Dk Efreim
Lema alisema kuwa zoezi hilo lipo kwa mujibu wa sheria na linalenga kudhibiti
magonjwa ya mifugo, kudhibiti wizi wa mifugo, kuboresha mazao ya mifugo kama
nyama kwa kuboresha soko la mifugo ndani na nje ya nchi.
Lema alieleza kuwa kufanyika kwa
zoezi hilo kutasababisha kupatikana kwa masoko maalumu kwa ajili ya
kuuza mifugo yao kwa bei nzuri na hivyo kukuza uchumi wao na taifa
kwa ujumla.
Aidha aliwataka wananchi na wafugaji
kupuuza uvumi unaonezwa kuwa serikali inapiga chapa mifugo hiyo ili kuitaifisha
na pia wataanza kulipia kodi baada ya
mifugo yao kutambuliwa.
Na kuongeza kuwa zoezi hilo halina
nia ya kukwamisha shughuli zozote za kimaendeleo ama serikali kuchukua mifugo ya
wafugaji kama inavyodaiwa na baadhi ya watu bali ni kuhakikisha inamwekea
mfugaji miundombinu ya kisasa ili aweze kufuga kwa tija kama nguzo
moja wapo ya kuimarisha uchumi wake na Taifa kwa ujumla.
Wilaya ya Maswa ndiyo wilaya pekee
iliyoanza kutklza zoezi hilo mkoani Simiyu na inatarajia kupiga chapa ng’ombe wapatao 445,732
katika Kata zote 36 zenye vijiji 120 ikiwa ni utekelezaji wa agizo la serikali
la kufanya utambuzi, usajili na ufuatiliaji wa mifugo.
Hata hivyo Upigaji chapa huo ni
agizo la kisheria kwa mujibu wa sheria Namba 12 ya mwaka 2010 ya Utambuzi na
Usajili sambamba na utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu,Kassim Majaliwa
alilolitoa hivi karibuni la kutaka kila mfugaji nchi nzima asajiliwe na mifugo
yake ipigwe chapa.
. Mifugo ikiandaliwa kupigwa chapa