NG’OMBE 445,732 KUPIGWA CHAPA MKOANI SIMIYU;
WILAYA ya Maswa mkoani Simiyu inatarajia kupiga chapa ng’ombe wapatao
445,732 katika Kata zote 36 zenye vijiji 120 vilivyoko katika wilaya
hiyo ikiwa ni utekelezaji wa agizo la serikali la kufanya
Upigaji chapa huo ni agizo la kisheria kwa mujibu wa sheria Namba 12
ya mwaka 2010 ya Utambuzi na Usajili sambamba na utekelezaji wa agizo
la Waziri Mkuu,Kassim Majaliwa alilolitoa hivi karibuni la kutaka kila
mfugaji nchi nzima asajiliwe na mifugo yake ipigwe chapa.
Hayo yalisema jana na Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya
Maswa,Mhandisi Ally Mubaraka kwa Waandishi wa habari katika kijiji cha
Shishiyu wilayani humo waliokuwa wakifuatilia zoezi hilo la upigaji
chapa katika kijiji hicho.
Alisema kuwa Utambuzi na Ufuatiliaji wa Mifugo ni mfumo unaowezesha
kuwa na alama na kumbukumbu ya mifugo kupitia usajili wa mifugo
yenyewe, wamiliki wake, mahali ilipo na matukio muhimu kwenye uhai wa
mifugo hiyo.
“Utambuzi wa mnyama unaweza kuwa wa mnyama mmoja mmoja au wa kundi kwa
maana ya alama moja kwa kundi la wanyama mfano hapa katika wilaya ya
Maswa utambuzi wa wanyama kwa kundi unafanyika kwa kila kijiji kuwa na
alama moja ya chapa ya utambulisho wa kitaifa,”alisema.
Alisema kuwa zoezi la kupiga chapa mifugo lipo kisheria kutokana na
sheria namba 12 ya mwaka 2010 ambapo mpango huo ni utekelezaji wa
sheria inayolenga wafugaji kupiga chapa mifugo yao sambamba na
kuorodheshwa mifugo yao katika daftari maalumu ili mwisho wa siku
iweze kubainika idadi kamili ya mifugo iliyopo katika wilaya nzima.
“Endapo mifugo haitapigwa chapa itachochea kuendelea kuwepo kwa
migogoro kati ya wakulima na wafugaji na pia kuwa na uwezekano mkubwa
wa kuingia mifugo mipya bila taarifa ndani ya wilaya,’’alisema.
Hata hivyo anabainisha kuwa serikali ina lengo la kuboresha
miundombinu ya wafugaji hususani majosho , malambo , masoko ya ndani
na nje ya nchi hivyo haina budi kujua idadi kamili ya mifugo iliyopo ,
nyama inayozalishwa na hata mfugaji mwenyewe aweze kujulikana .
Aidha Mhandisi Mubaraka alibainisha kuwa zoezi hilo linaendeshwa kwa
wafugaji katika vijiji vyote ndani ya wilaya hiyo na kuwataka
wafugaji kujitokeza zaidi katika kufanikisha zoezi hilo.
Alisema kuwa endapo mifugo hiyo itapigwa chapa hususani ng’ombe
itapelekea kuwepo kwa mazingira mazuri ya malisho,kupata maji, nyama
kuuza katika masoko mazuri sambamba kuzalisha zaidi mifugo.
Pia aliwataka viongozi wa vijiji , viongozi wawakilishi wa wafugaji
,maafisa mifugo kuwahamasiaha wafugaji kujitokeza katika zoezi
hilo la kupiga chapa mifugo kwani zoezi hilo lina manufaa kwao na ni
agizo la serikali.
Hata hivyo anatoa onyo kwa wale watakaokaidi agizo la kupiga chapa
mifugo yao watatozwa faini ya kiasi cha shilingi milioni 2 ama kifungo
cha miezi sita kwani wanakiuka agizo zuri la serikali.
Naye Afisa Mifugo wa Wilaya hiyo,Dk Efreim Lema alisema kuwa lengo la
kuwepo kwa zoezi hilo ambalo lipo kwa mujibu wa sheria linalenga
kudhibiti magonjwa ya mifugo,kudhibiti wizi wa mifugo,kuboresha
mazao ya mifugo nyama na mazao sambamba na kuboresha soko la mifugo
ndani na nje ya nchi.
Lema alieleza kuwa kufanyika kwa zoezi hilo kutasababisha kupatikana
kwa masoko maalumu kwa ajili ya kuuza mifugo yao kwa bei nzuri na
hivyo kukuza uchumi wao na taifa kwa ujumla.
‘Zoezi hili linafanyika hivyo kuna sehemu maalumu ya kupiga chapa
kwenye mwili wa ng’ombe ambapo ni mguu wa nyuma kulia chini ya paja
ambapo ngombe kuanzia umri wa miezi 6 hadi 12 anaweza kupigwa chapa
bila ya kupata madhara yoyote ama kujali ana umri mdogo ama mkubwa,”.
“Niwaondoe hofu wafugaji kuwa hata ndama mwenye umri huo anaweza
kupigwa chapa sawa na wale ng’ombe wenye umri mkubwa bila ya kupata
madhara yoyote yale na kila ng’ombe mmoja atatozwa Sh 500 ili
kuchangia gharama za zoezi la chapa.’’alisema.
Hata hivyo alisema kuwa zoezi hilo halina nia ya kukwamisha shughuli
zozote za kimaendeleo ama serikali kuchukua mifugo ya wafugaji kama
inavyodaiwa na baadhi ya watu bali ni kuhakikisha inamwekea mfugaji
miundombinu ya kisasa ili aweze kufuga kwa tija kama nguzo moja wapo
ya kuimarisha uchumi wake na Taifa kwa ujumla.