KIWANDA KIKUBWA CHA CHAKI KUJENGWA MASWA.
Na mwandishi wa MAKALIBLOG.
COSTANTINE MATHIAS; SIMIYU.
KUFUATIA Agizo la Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Dr. John Pombe Magufuli la kuwa na Tanzania ya Viwanda,
Mkoa wa Simiyu unatarajia kujenga kiwanda kikubwa cha chaki kikiwa na
teknolojia mpya katika Ukanda wa Afrika Mashariki ambacho kitasaidia kuongeza ajira
na kukuza uchumi wa mkoa na taifa kwa ujumla.
kiwanda hicho ambacho kitakuwa
na teknolojia ya kisasa zaidi katika uchanganyaji unga, uzalishaji na
ufungashaji kitaongeza ajira kwa vijana wilayani Maswa ambao alikuwa wameanza
na kiwanda kidogo kilichokuwa kikizalisha kwa kutumia teknolojia duni.
Hayo yalibainishwa jana na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Anthony Mtaka katika Kikao cha Baraza la Madiwani mjini Maswa wakati akifafanua mikakati ya mkoa katika kutekeleza azma ya serikali ya viwanda.
Mtaka alisema kuwa kwa kuwa kiwanda kikubwa kinatarajiwa kujengwa Maswa Halmashauri ianze kufikiria kumiliki vitalu vyake vya chokaa ambapo hadi sasa wanamiliki ekari 20 ambazo zitasaidia kulisha kiwanda hicho wakati wa uzalishaji ili kisikose malighafi.
‘’tunajenga kiwanda kipya kikubwa
cha chaki na cha kisasa ambacho hakipo Afrika Mashariki…na shilingi milioni 50
zimeshatolewa na UNDP kwa ajili ya upembuzi yakinifu’’ alisema Mtaka.
Aliongeza kuwa kiwanda hicho
kitakuwa na teknolojia ya kisasa katika uzalishaji wake huku ujenzi wake
utagharimu zaidi ya shilingi bilioni 1.5 zilizotolewa na mfuko wa Hifadhi ya
jamii (NSSF).
Aidha Mtaka ameziagiza halmashauri
zote mkoani hapa kubuni vyanzo vipya vya mapato hasa kwa kuanzisha
viwanda vidogovidogo na vikubwa ili waachana na tabia ya kuwatoza ushuru
wakulima wakulima wa mazao mashambani.
‘’halmashauri zibuni vyanzo vipya
vya mapato na siyo kufikiria kutoza ushuru wauza michicha na nyanya
sokoni…mfano halmshauri ya Maswa leo imepokea milioni 70 toka Zanzibar baada ya
kuuza chaki na bado wanadai milioni 200’’ alisisitiza Mtaka.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa
Halmashauri ya Wilaya ya Maswa Dr. Fredrick Sagamiko alisema kuwa hadi sasa
wilaya yake imeanza mchakato wa ujenzi wa kiwanda cha kuongeza thamani ya mazao
ya ngozi.
Alisema kuwa kiwanda hicho kinajengwa
katika kijiji cha Senani chini ya ubia wa wajasiriamali Kijijini hapo, Chuo
Kikuu cha Sokoine cha Kilimo-SUA na Chuo cha Teknolojia -DIT ambapo ujenzi
wake utakamilika mwezi Julai mwaka huu.
‘’ujenzi wa kiwanda cha kuongeza
thamani ya mazao ya ngozi unandelea, pia tumeanza kusajili na kutambua mifugo
yote wilayani maswa ambapo wananchi wameitikia zoezi la upigaji chapa mifugo
yao’’ alisema Sagamiko.
Aidha Kwa upande wao wananchi wamesema
kuwa agizo la Mkuu wa mkoa la kufutwa kwa ushuru wa mazao litasaidia
halmashauri kubuni miradi na vyanzo vingine vya mapato kuliko kutegemea ushuru
wa sokoni.
‘’ni kweli watasaidia hata wataalamu
kubuni miradi ambayo itakuwa vyanzo vya mapatoa katika halmashauri kuliko
kutegemea ushuru wa minadani, sokoni, mazao na stendi’’ alisema Juma Ally.
MWISHO