CCM YAMSHANGAA LOWASSA KAULI YA KUTUMA 'MTOTO MDOGO' MAZISHI YA WANAFUNZI LUCKY VICENT

Chama cha Mapinduzi mkoa wa Arusha kimeishangaa kauli ya aliyekuwa
Waziri Mkuu Edward Lowassa kusema kuwa Rais John Magufuli amemtuma
‘mtoto mdogo’ kwenda kuiwakilisha serikali kwenye mazishi ya wanafunzi
wa shule ya Lucky Vicent.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mwenyekiti wa CCM mkoa wa
Arusha Michael Lekule ,alisema kauli ya Waziri huyo mstaafu ameitoa kwa
kudanganya wananchi na kuonesha serikali ya Magufuli haishirikiani na
wananchi ,wakati serikali iliubeba msiba huo mzito wa taifa.
Alisema jitihada za serikali ya Magufuli zimeonekana kupitia kwa
wawakilishi wake Makamu wa Rais Samia Suluhu pamoja na Mrisho Gambo
pamoja na wanachama wa CCM ambao walijitokeza kwa wingi kwenye msiba huo
mzito
"Serikali ilijitoa kwa hali na mali kuwezesha familia 35 kwenda
kupumzisha wapendwa wao,na ilihakikisha kila mwili unapumzika mahala
popote familia inapopata,tunajiuliza walitaka nini kama kote nafasi
ilijazwa na serikali ya Magufuli," alisema Michael
"CCM inakanusha kwanguvu upotoshaji huo,hata ukiangalia siku ile uwanja
wa shekh Amri Abeid wanaccm walijaa uwanjani ,kikubwa CCM imeguswa na
msiba uliotokea na Rais wetu amekuwa bega kwa bega juu ya tukio
lililotokea,"alisema
Pia alisema wamemshangaa kwa kusema Rais alimtuma mtoto mdogo wakati
yeye mwaka 2007 ajali mbaya iliyotokea Monduli duka bovu na kuua watu 20
ambao 11 walikuwa ni askari wa JKT,rais Kikwete alimtuma aje
kuiwakilisha serikali.
Hata hivyo alimtaka kiongozi huyo, ajiulize kama yeye kipindi akiwa
Waziri Mkuu aliweza kutumwa na Rais, amuwakilishe kwenye msiba wa watu
20, je yeye na Makamu wa Rais ni nani mdogo?
"Tena ajali hiyo ilikuwa ya kitaifa,askari 11 walifariki kwenye ajali,mbona hajayasema ya kwake?," alisema Lekule