Ongeza Uwezo Wako Wa Kupata Pesa Kwa Kufanya Mambo Haya...!!!
Upo uwezekano mkubwa wa wewe kuongeza uwezo wako wa kupata pesa zaidi ya
hapo ulipo ikiwa utafuata misingi sahihi ya pesa jinsi inavyotaka. Kila
kitu kina kanuni zake ikiwamo hata kanuni za kupata pesa.
Kama bado unashangaa kwa nini wengine wana pesa nyingi na wewe huna,
hiyo yote ni kwa sababu wanazifanyia kazi kanuni za pesa bila kujali
wanazitumia kwa bahati mbaya au kwa kujua.
Huna haja ya kuendelea kukosa pesa kila wakati. Umefika wakati wa
kukubali kujifunza na kutumia kanuni za pesa ili zikusaidie kuongeza
uwezo wako wa kupata pesa na kufanikiwa maishani mwako.
Kupitia makala haya, naomba nikuachie dondoo kadhaa zitakazoweza
kukusaidia moja kwa moja kuongeza uwezo wako wa kupata pesa na kuwa mtu
wa mafanikio. Karibu tujifunze kwa pamoja;-
1. Jifunze mambo ya pesa kila siku.
Jifunze kwenye vitabu, pia jifunze kwenye semina. Huwezi kufanikiwa
kipesa kama hujachukua hatua za kujifunza jinsi pesa inavyofanya kazi.
Unalazimika kujua jinsi pesa inavyoweza ikawekezwa na kudumu katika
maisha yako. Yote haya hayawezi kuja kwenye upande wako kama uchawi bali
ni kwa wewe kuweza kujifunza.
2. Tafuta mshauri (Mentors) atakayekuwa anakuongoza kwenye mambo
yako ya pesa pale unapokwama au unataka kusonga mbele zaidi. Hili
linaweza kuwa jambo ni dogo kwako lakini ni muhimu kwako.
Watu karibu wote ambao wana mafanikio kila siku wana watu ambao
wanawafuata au wanawashauri kila mara katika mambo ya pesa. Hali hiyo
hupelekea kuwaweka juu kimafanikio.
3. Kama upo kwenye madeni, tafuta namna ya kuondoka huko. Madeni
ni sumu kubwa ya mafanikio kama utakuwa nayo kwa muda mrefu. Kama una
madeni mengi, upo uwezekano wa nidhamu yako ya kipesa ikawa mbovu.
Weka mpango imara ambayo itaweza kukutoa kwenye madeni na kuanza kuishi
kwa uhuru wa kifedha. Hutaweza kufika mbali kimafanikio ikiwa kila
wakati ni mtu wa kudaiwa, hutaweza kufanya kitu chochote.
4. Jilipe wewe kwanza kila ukipata pesa yoyote ile. Kila aina ya
pesa unayoipata, tenga kiasi kidogo na ujilipe kama mtafutaji wake.
Usiache kujilipa hata kama pesa uliyopata ni kidogo.
Pesa ile ambayo utakuwa unajilipa wewe kwanza, huna haja ya kuwa nayo na
haraka kuitumia. Kama ambavyo tumekuwa tukisema iache iwe nyingi baada
ya hapo iwekeze.
5. Tafuta namna pesa zako zitakavyoweza kukulinda pale unapokuwa
umeumia au kufa na kuacha watoto wadogo. Kuwa na ulinzi wako kama bima
vile, lakini wewe bima yako inaweza ikawa pia vitega uchumi vyako
mbalimbali.
Hapa unatakiwa ujifunze kuwekeza mapema wakati bado ukijana mwenye
nguvu. Kwa kadri jinsi unavyozidi kuwekeza pesa zako zitakulinda hata
pale utakopokuwa umeshazeeka au kupatwa na matatizo yoyote.
Hivyo ndivyo unavyoweza kuongeza uwezo wako wa kupata pesa kama
utazingatia mambo hayo matano kama yalivyowekwa wazi kupitia makala
haya. Naamini umejifunza kitu na chukua hatua.