Zitto Kabwe Amtaka Rais Magufuli Avunje Bunge
Mbunge
wa Kigoma Mjini Zitto Kabwe amemshauri Rais wa Tanzania Dkt. John
Magufuli kulivunja Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania endapo
analiona ni kikwazo kwake.
Ushauri
huo ameutoa jana ikiwa ni saa chache baada ya Rais Magufuli kukosoa
uamuzi wa Bunge kumuita Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda
kujieleza mbele ya Kamati ya Bunge, kutokana na kilichodaiwa na wabunge
kuwa ni kauli ya kulidhalilisha Bunge.
Katika
hotuba yake aliyoitoa jana wakati wa kuapishwa kwa Kamishna Mkuu wa
Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya, Rais Magufuli
aliwataka viongozi wengine kumuunga mkono mtu anayejitokeza kupiga vita
dawa za kulevya badala ya kumdhalilisha.
"Tunapomuona
mtu anajitokeza kupambana na haya madawa ya kulevya, badala ya
kumdhalilisha tumuombee na kumtia moyo, hawa wanaweza hata kubadilisha
maneno uliyoyazungumza wakabadilisha wakatengeneza kwenye clip wakatupa,
na wakajitokeza wengine wakasema wameingilia mamlaka yao, wakati wao
wanaingilia mamlaka ya kuwaita wengine, hii ni vita". Alisema Magufuli
Baada
ya kauli hiyo ya Rais, Zitto kupitia ukurasa wake wa Facebook ameonesha
kushangazwa na kile alichodai kuwa Rais hakujua kuwa sheria ya kuundwa
kwa mamlaka hiyo, ilitungwa, na kwamba anashangaa kuona Rais hakuwa
akijua kuwa alipaswa kumteua Kamishna Mkuu wa Mamlaka hiyo
Ujumbe wa Zitto unasema
"Wabunge
walitoa Hoja Binafsi kuhusu Madawa ya kulevya ( Esther Bulaya na
Faustine Ndugulile ) na kufuatia hoja hiyo Serikali ikaleta Muswada
bungeni na Bunge likatunga Sheria ya Kupambana na Madawa ya kulevya
mwaka 2015.
"Serikali
mpya ikaingia madarakani mwezi Novemba 2015. February 2017 Ndio
Kamishna Mkuu anateuliwa tena baada ya wabunge kuhoji na kushinikiza
kupitia Kamati husika na pia mbunge Esther Bulaya aliyetoa Hoja Binafsi
katika Bunge la Kumi.
"Rais
anasema hakuwa anajua kuwa sheria hiyo ipo. Lakini Rais anapogawa
Wizara huwa anatoa instruments na Hizo instruments hutaja kila sheria
kwa kila Waziri. Ilikuwaje Rais akasahau sheria hii nyeti kama alikuwa
na nia ya dhati ya Kupambana na Madawa ya kulevya?
Rais
anaona Bunge kikwazo kwa sababu Bunge linamwongoza afuate sheria.
Lakini Kama anaona Bunge linamkera turudi kwenye uchaguzi tu, alivunje".