Zitto Kabwe: “Buriani Babu Samwel John Sitta”
Ujumbe maalum alioutuma Mh. Zitto Kabwe mapema jana kufuatia kifo cha Mzee Samweli Sitta kilichotokea huko Ujerumani.
“Alfajiri
ya , Novemba 7, 2016 imekuwa siku ya huzuni na majonzi makubwa kwa
Taifa. Tuliamka na kukutana na habari za kusikitisha juu ya kifo cha
Mzee wetu Samwel John Sitta, Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania. Mzee Sitta alikuwa mgonjwa kwa kitambo kidogo,
lakini bado tulikuwa na matumaini kuwa afya yake ingetengamaa na
kuendelea kuwa nasi.
Habari
hizi za kufariki dunia kwake zilizosambaa kwa kasi kubwa kupitia
mitandao ya kijamii zimetushtusha mno. Hatimaye taarifa rasmi ikatoka
kuthibitisha habari hizo. Kuwa Mzee watu amefariki dunia akiwa kwenye
matibabu nchini Ujerumani.
Samwel
John Sitta aliitumikia nchi yetu kwa muda mrefu na kwa uadilifu mkubwa
sana. Si hivyo tu, sisi wengine pia kwa kiasi flani Hata kukua kwetu
kisiasa kumetokana na utumishi wake uliotukuka kwa nchi yetu alipokuwa
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Katika tanzia hii
ninamkumbuka Mzee Sitta Kwa namna nilivyofungamana naye binafsi na namna
nilivyomshuhudia katika kazi zake mbalimbali za uongozi.
Samwel
Sitta ananigusa mimi binafsi moja kwa moja. Alikuwa Babu yangu. Tukiwa
Bungeni akiniandikia kitu alikuwa akitumia neno hilo ‘babu’ kwa mwandiko
wake mzuri usiotoka kwenye kumbukumbu zangu kabisa. Labda siku za usoni
‘vinote’ (vimemo) hivi vinaweza kuchapishwa pindi watafiti watakapokuwa
wakiandika historia ya nchi yetu na Bunge letu. Hivyo siku zote za
maisha yetu nilimuita babu.
Disemba
29, 2005 mzee Sitta aliniapisha kiapo cha ubunge tarehe. Maneno ambayo
aliniambia baada ya kunikabidhi Kanuni za Bunge na Katiba ya Nchi
niliyaandika kwenye daftari langu la kumbukumbu siku hiyo hiyo jioni.
Baada ya kula kiapo cha Utii na cha uaminifu kawaida Wabunge hupewa
mkono na mwapishaji na kupewa nyaraka za kazi.
Kwangu
haikuwa hivyo, Mzee Sitta alinikumbatia na kuniambia “Utakuwa Kiongozi
muhimu sana kwa nchi yetu. You have a bright future (unayo kesho
njema)”. Maneno haya hayajawahi kunitoka katika kumbukumbu zangu, ni
maneno ya faraja na msukumo wa kunitaka kwenda mbele kila ninapopata
misukosuko ya kisiasa. Mara kadhaa yeye mwenyewe alikuwa akinipigia na
kunikumbusha juu ya maneno yake haya na kunitia moyo.
Babu
Sitta alikuwa Mlezi wa wanasiasa vijana, binafsi amenilea na
kunisomesha. Mwaka 1996 nilikuwa mwanafunzi wa Kidato cha Tano (Form
Five) katika Shule ya Sekondari ya Galanos ya jijini Tanga, nikisomea
mchepuo wa Historia, Jiografia na Uchumi (HGE). Hali ya hewa ya jiji la
Tanga haikunipenda, hivyo nikawa naumwa mara kwa mara.
Lakini
pia sikupenda kusoma HGE, nilitaka kusoma Hisabati badala ya Historia.
Wakati wa likizo ya mwezi Disemba mwaka 1996, nilitoka Tanga nikaenda
Dar es Salaam, Wizara ya Elimu kuomba uhamisho kwenda shule yenye Somo
la Hisabati kidato cha Tano na Sita. Nikakataliwa. Lakini nikaambiwa
kuwa Mkurugenzi wa Elimu ya Sekondari wakati ule, ndugu Ndeki alisoma
pamoja na Samwel Sitta.
Kipindi
hicho Mzee Sitta akiwa Mkurugenzi wa Investments Promotion Centre (IPC)
mara kabla haijabadilishwa jina kuwa Tanzania Investments Centre (TIC)
mara baada ya kuwa mbunge wa Urambo kwa miaka 20 (1975 – 1995). Nikaenda
Ofisi za IPC, zilizokuwa mahala ambapo leo ni Benki ya CRDB Tawi la
Azikiwe. Nilipofika Katibu Muhtasi wake akaniuliza kama nina miadi na
bosi wake, nikasema hapana. Akaniambia hawezi kukuona. Nikasisitiza sana
na kumlilia dada yule aniruhusu hata kwa akika chache tu. Akaniruhusu.
Nilipofika
Mzee Sitta aliniuliza shida zangu kwa heshima kubwa. Nikamwambia kwamba
ninataka kuhama shule. Akaniomba matokeo yangu ya Kidato cha Nne,
nikampa maana nilikuwa natembea nayo. Alipoyasoma akaniambia, “wewe
hupaswi kuhangaika kutafuta shule maana kwa matokeo yako unaweza kusoma
shule yeyote nchini ya chaguo lako”. Akainua simu akampigia ndugu Ndeki
kumuomba anihamishe.
Kisha
akaniandikia kikaratasi niende Wizarani muda ule ule. Nilipofika
Wizarani nikapewa uhamisho kwenda Shule ya Sekondari Mazengo. Nilipotoka
nje ya Wizara nikakutana na kijana mwengine, Godfrey Hiluka, anaomba
uhamisho, yeye anatoka Mazengo anataka kwenda Tosamaganga Iringa.
Akaniambia, achana na Mazengo hakuna Mwalimu wa Uchumi na hali ya vyoo
ni mbaya sana.
Nikarudi
kwa Mkurugenzi. Mtumishi aliyenijazia fomu za Uhamisho (Mzee wa Makamo)
aliponiona narudi na kumwambia sitaki kwenda Mazengo, akachukua fomu
zangu za uhamisho na akachukua ‘kifuta – wino’ (whiteout) akafuta
Mazengo na kuweka Tosamaganga huku akisema kwa hasira “nyie watoto wa
wakubwa bwana!”Sikujali nikaenda zangu Tosamaganga kusoma Uchumi,
Jiografia na Hisabati (EGM).
Samwel
John Sitta akaendelea kufuatilia maendeleo yangu shuleni, mpaka Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam na baadaye Taasisi ya InWent nchini Ujerumani.
Nilipotoka Ujerumani kusoma masomo ya Juu ya Biashara ya Kimataifa mwaka
2004 nilipaswa niwe na mradi wa kitaaluma. Nikachagua kuunganisha
makampuni ya Kijerumani na makampuni ya Tanzania kwa kuandika mradi wa
kuchukua wafanyabishiara 20 kutoka Tanzania na kuwaunganisha na wengine
20 kutoka nchi za Jumuiya ya Ulaya.
Ilibidi
kupata Taasisi ya Tanzania kwa ajili mradi huo na Mzee Sitta akawa
mstari mbele kuhakikisha Mradi unafanikiwa na tukautekeleza kwa umakini
kwa msaada wa afisa wa TIC aitwaye Phina Lyimo. Mafungamano yetu
hayakuishia hapo, mwaka mmoja baadaye tukakutana na Mzee Sitta Bungeni,
yeye akiwa Mbunge wa Jimbo la Urambo Mashariki na mimi nikiwa Mbunge wa
Jimbo la Kigoma Kaskazini. Ulezi wake kwangu ukaendelea mpaka mauti
yalipomkuta leo mapema asubuhi. Taifa limepoteza Kiongozi mzalendo,
lakini mimi nimepoteza pia ‘babu Mlezi’.
Samwel
John Sitta alikuwa Mwanamageuzi (Reformer), na kupitia uanamageuzi wake
alifanya mabadiliko makubwa sana katika uendeshaji wa shughuli za Bunge
akiwa Spika wa Bunge kwa miaka mitano. Sisi tuliohudumu kwenye Bunge la
tisa chini yake, tukimwita Spika wa Viwango na Kasi, tuliona wenyewe
juhudi zake za kuliweka Bunge katika nafasi yake ya Kikatiba.
Licha
ya kuhakikisha kuwa maslahi ya Wabunge yanakuwa yanayolingana na hadhi
ya Bunge, alihakikisha pia kuwa Bunge linaisimamia Serikali sawa sawa.
Haikuwa kazi rahisi sana kwani kulikuwa na mvutano mkubwa sana kati ya
Spika Sitta na Waziri Mkuu Edward Lowasa katika kuleta mabadiliko hayo.
Tulikuwa
tunaambiwa kuwa mvutano ule ulitokana na tetesi kwamba Sitta ndiye
alipaswa kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na hivyo
kuwa na msuguano na aliyeteuliwa kushika nafasi hiyo badala yake. Sio
Sitta wala Lowasa ambaye alithibitisha ama kukanusha tetesi zile. Sitta
ametangulia mbele ya haki, labda Edward Lowasa ataweza kusemea hili siku
za usoni.
Samwel
Sitta alitumia fursa ya msuguano huo kufanya mabadiliko makubwa ya
kanuni za Bunge na kutoa uhuru mpana wa mawazo ndani ya Bunge na
kuhakikisha kuwa Taarifa za Kamati za Bunge, hususan Kamati za Usimamizi
wa Serikali, zinakuwa zinasomwa na kujadiliwa ndani ya Bunge kwa mujibu
wa Kanuni.
Wakati
wa Bunge la 8 chini ya mzee Pius Msekwa, Taarifa za CAG hazikuwahi
kusomwa hata mara moja bungeni. Ni kutokana na mabadiliko haya ya kanuni
ndipo Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC )
ilianzishwa mwezi Machi, mwaka 2008. Nilichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa
kwanza wa Kamati ile na kuingia kwenye Kamati ya Uongozi ya Bunge ambayo
kipindi hicho tuliiona kama Kamati ya Wabunge wazee.
Namna
nilivyoingia kuwa Mwenyekiti wa POAC nayo ni hadithi nyengine ya namna
ya malezi ya kiuongozi yalifanywa na Spika Sitta. Sikuwa nimejaza fomu
kuomba hata ujumbe wa Kamati ya POAC. Wakati huo ulikuwa ni wakati wa
vuguvugu la Buzwagi (Mkataba wa Madini uliosainiwa na Waziri wa Nishati
Hotelini nchini Uingereza kwa siri).
Nilikuwa
mjini Bagamoyo kwenye kazi za Kamati ya Bomani (Kamati iliyoundwa na
Rais kuchunguza mikataba na sheria za madini) nikiwa na Harrison
Mwakyembe na Ezekiel Maige. Spika wa Bunge akanipigia simu, akaniambia
“Babu, kesho kuna uchaguzi wa Kamati za Bunge. Nimekuteua Kamati ya POAC
ambayo ni Kamati mpya itakayokuwa chini ya Kambi ya Upinzani.
Najua hukuomba kuwa mjumbe wa Kamati hii, lakini nahitaji damu changa
kwenye Kamati ya Uongozi ya Bunge. Naomba unikubalie na kesho uwepo Dar
es Salaam kwa ajili ya uchaguzi na ugombee. Utashinda maana nimeshafanya
kazi yangu”.
Sikuwa
na namna ya kukataa japo nilitaka sana kuendelea kuwa mjumbe wa Kamati
ya Fedha na Uchumi chini ya marehemu Abdallah Kigoda, ama Kamati ya
Nishati na Madini chini ya Mzee William Shelukindo. Lakini ombi la Mzee
ni amri. Nikawa Mwenyekiti wa POAC na kuwa mmoja wa washauri wakuu wa
Spika wa Bunge. Kamati ya PAC ikawa chini ya Mzee John Momose Cheyo na
Kamati ya LAAC ikawa chini ya Dkt. Willibrod Peter Slaa. Ilikuwa ni
Bunge lenye meno kweli kweli.
Spika
Sitta alikuwa mbabe. Ubabe wake ulimpelekea kufanya maamuzi ambayo
wakati mwengine yalimweka kwenye matatizo na wananchi. Mfano mzuri ni
masuala ya ‘Hoja Binafsi ya Buzwagi’ na ‘Hoja ya Wizi wa Fedha Benki Kuu
(EPA)’. Mwanzoni, Spika alikuwa upande wa Wabunge wenye hoja hizo,
yaani mimi na Dkt.
Wilbroad
Slaa kiasi cha kuziboresha hoja zile kwa kalamu yake mwenyewe. Wabunge
wa chama chake hawakuwa wanapenda hoja hizi na hivyo Waziri Mkuu Edward
Lowasa akamweka kwenye wakati mgumu sana wa kuegemea upande wa Serikali.
Hoja
ya dkt Slaa akaitupa kuwa ‘Ni makaratasi ya kuokoteza’. Hoja yangu
akaiingiza Bungeni na akasimamia kusimamishwa kwangu Bungeni baada ya
kuwasilisha hoja hiyo. Wananchi walimkasirikia sana. Siku moja usiku,
nikiwa nyumbani kwa ndugu Freeman Mbowe Mikocheni, Spika Sitta
akanipigia simu kulalamika kuwa wafuasi wangu wanamtukana kwa ujumbe wa
simu (sms), akanitaka niwakataze. Nilimkubalia tu, lakini sikuwa na
uwezo huo. Nchi ilikuwa imevimba. Ilikuwa Oktoba 2007. Samwel Sitta
alijua namna ya kuisoma nchi, na akamua kuwapa wananchi watakacho,
wakati mwengine.
Mwezi
Novemba, katika kujibu kiu ya wananchi kuhusu uwajibikaji na kufuta
makosa ya Buzwagi na EPA, Spika alisimamia kuundwa kwa Kamati Teule
kuchunguza suala la Mkataba wa Richmond. Yaliyofuata yalikuwa historia.
Taarifa ya Kamati Teule husika ilipelekea kuanguka kwa Serikali kwa mara
ya kwanza katika hsitoria ya Tanzania.
Waziri Mkuu Edward Lowasa alilazimika kujiuzulu ndani ya Bunge, Baraza
la Mawaziri likavunjika na Serikali mpya kuundwa chini ya Waziri Mkuu
mpya, ndugu Mizengo Pinda. Spika Samwel Sitta akawa ni Spika wa pili wa
nchi yetu aliyeshuhudia uundwaji wa Serikali mbili ndani ya miaka mitano
ya uspika wake.
Mzee
Msekwa yeye alikaa kwenye Uspika kwa miaka 13. Miaka 10 na Waziri Mkuu
mmoja, ndugu Sumaye. Akianzia Uspika Mwaka 1993. Mwaka mmoja mbele
akishuhudia mabadiliko ya Mawaziri Wakuu, kutoka mzee John Malecela
kwenda kwa mzee Cleopa Msuya. Baada ya kujiuzulu kwa Lowasa, Samwel
Sitta hakurudi nyuma tena. Aliendelea kuwa Spika wa Viwango mpaka
alipomaliza muda wake katika Bunge la Tisa.
Sifa
nyengine ya Spika Sitta ni Uungwana, alikuwa mwepesi mno wa kuomba
msamaha pale alipokosea. Nakumbuka siku moja mwaka 2009 alimfukuza
Bungeni Mzee mwenzake John Cheyo kwa makosa ambayo Mzee Cheyo hakufanya.
Baadhi yetu tukakasirishwa sana na kitendo kile.
Nikaenda
kumwona Mzee Sitta ofisini kumwuliza kulikoni amdhalilishe mwenzake
namna ile. Akanieleza kuwa hakuwa sawa na atamwomba radhi John Cheyo.
Tukiwa kwenye Kamati ya Uongozi ya Bunge, kwa ajenda zake za kawaida tu,
Mzee Sitta akamwomba radhi Mzee Cheyo.
Nikikumbuka
kisa hiki hutabasamu, maana Jaji Werema, aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa
Serikali alicheka mpaka kuanguka chini. Sababu? Mzee Sitta aliketi
kwenye kiti chake, wenyeviti wote wa Kamati tukiwa tumetulia tuanze
kikao. Mzee Sitta akasema “John, naomba radhi kwa tukio lililotokea
Bungeni wiki iliyopita. Sijui nilikuwa nina nini siku hiyo?, nadhani
nilisumbuliwa na watu wanaopitapita jimboni kutaka kunitoa, nisamehe
Mzee mwenzangu”.
Kicheko
ukumbi mzima na mzee John Cheyo akamkubalia radhi yake huku naye
akicheka na yakaishia hapo. Wazee hawa wawili wameandika pamoja Kitabu
“Bunge lenye Meno”.
Nimwelezeje
zaidi Babu? Nimwelezeje zaidi Spika wa Kasi na Viwango Samwel John
Sitta? Mwanasiasa Shupavu, Jasiri, Mwenye Ngozi Ngumu, Mbabe,
Mnyenyekevu inapobidi na mwenye Uthubutu. Tangulia Babu. Tangulia Mjukuu
wa Fundikira. Tangulia Mtemi wa Unyanyembe Samwel John Sitta. Ingawa
umeondoka duniani, bado unaishi kupitia kazi zako za Kizalendo kwa Nchi
yetu.” “
Kabwe Z. Ruyagwa Zitto
Novemba 7, 2016
Dodoma
Zitto