ASKARI POLISI 152 WAFUKUZWA KAZI TANZANIA
Jumla
ya askari 152 wamefukuzwa kazi mwaka huu na Jeshi la Polisi kwa sababu
ya kukiuka Sheria, Taratibu na Kanuni ya Jeshi hilo kama zilivyoainishwa
katika Kanuni za Kudumu za Polisi (PGO) namba 103.
Idadi ya askari hao waliofukuzwa kazi imetolewa jana
mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad
Masauni alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Mhe. Maryam
Msabaha aliyehitaji kufahamu juu ya idadi ya askari waliochukuliwa hatua
kwa sababu ya utovu wa nidhamu.
Mhandisi Masauni alisema
kuwa kazi ya Vikosi vya Ulinzi na Usalama ni kulinda raia, mali zao
pamoja na mipaka ya nchi lakini kuna baadhi ya askari hao wanakwenda
kinyume na Sheria kwa kuwapiga wananchi na kuwasababishia ulemavu pamoja
na vifo hivyo Jeshi hilo limewachukulia hatua za kinidhamu.
“Jeshi
la Polisi hufanya kazi kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na Taratibu
zilizopo lakini kuna baadhi ya askari wamekuwa wakikiuka maadili na
mwenendo mwema wa Jeshi letu hivyo kuanzia Januari 2015 hadi Juni 2016
tuliwachukulia hatua za kinidhamu askari 200”, alisema Mhandisi Masauni.
Naibu Waziri huyo alifafanua
kuwa baada ya askari hao kuchukuliwa hatua za kinidhamu, walifanyiwa
uchunguzi wa kina na jumla ya askari 152 kati ya 200 walikutwa na hatia
hivyo hatua iliyofata ni kuwafukuza kazi.
Akizungumzia kuhusu mpango wa Serikali juu ya kujenga nyumba za askari Polisi, Mhandisi Masauni alisema
kuwa wanatambua tatizo la makazi ya Askari Polisi katika maeneo
mbalimbali nchini hususani kwenye mikoa mipya hivyo Serikali ina nia ya
kutatua tatizo hilo kwa kuanza ujenzi wa nyumba kwa ajili ya askari hao.
“Serikali
imedhamiria kupunguza tatizo la upungufu wa makazi ya askari polisi kwa
kujenga nyumba kwa awamu kupitia mpango wa ujenzi wa nyumba 4,136 nchi
nzima ambao utaanza kutekelezwa baada ya taratibu za mkopo wa kuwezesha
ujenzi huu kukamilika”, aliongeza Mhandisi Masauni.