Wasichana wa Ifakara waiomba Serikali kuongeza adhabu kwa wanaosababisha mimba za utotoni
Wasichana
wanaoishi Ifakara, Wilaya ya Kilombero, Mkoani Morogoro wameiomba
Serikali kuongeza adhabu kwa wanaume wanaosababisha mimba za utotoni ili
kukomesha tatizo hilo.
Maombi
hayo yametolewa leo na Mwanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Ifakara
Jackline Mwalusako ambaye amekaimu nafasi ya Meneja Miradi wa Shirika la
Plan International- Ifakara kama ishara ya kuadhimisha Siku ya Msichana
Duniani itakayofanyika Oktoba 11 mwaka huu.
Mwalusako
amesema kuwa mila potofu pamoja na ndoa za utotoni ndio chanzo kikubwa
kinachosababisha kuongezeka kwa mimba za utotoni kwahiyo kuna haja ya
kubuni mbinu mpya zitakazotokomeza tatizo hilo.
“Pamoja
na adhabu zilizowekwa kwa ajili ya kuwaadhibu wanaume wanaosababisha
mimba za utotoni bado idadi ya wasichana wanaopata mimba za utotoni
inaongezeka, hivyo tunaiomba Serikali iwaongezee adhabu wanaofanya
makosa hayo ili kuzuia tatizo hili”, alisema Mwalusako.
Mwalusako
ameongeza kuwa wazazi pia wanachangia wasichana kupata mimba za utotoni
kwani wanakubali kuwaozesha watoto wao wakiwa bado wadogo kwahiyo nao
wanatakiwa kupewa adhabu ili waachane na tabia ya kuwaozesha kabla ya
muda muafaka.
Kwa
upande wake mwanafunzi anayekaimu nafasi ya Mratibu wa Miradi ya
Shirika la Plan International, Deborah Mtiko ametoa rai kwa shule
mbalimbali kuongeza utoaji wa elimu kuhusu mimba za utotoni ili kuwapa
uelewa wasichana waliopo mashuleni.
Mkoani
Morogoro, Shirika la Plan International – Tanzania linaadhimisha Siku
ya Msichana Duniani katika Kijiji cha Ihenga kilichopo mkoani humo
kuanzia saa tatu kamili asubuhi.