Wadau wa haki za binadamu nchini waendelea kusisitiza adhabu ya kifo ifutwe
Licha
ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutokeleza adhabu ya
kifo kwa zaidi ya miaka 20. Imeendelea kusisitizwa kuifuta sheria ya
adhabu ya kifo kwa watuhumiwa wa makosa ya mauaji kwa kuwa haisaidii
kupunguza makosa hayo na kwamba iangalie chanzo cha tatizo hilo kwa
lengo la kufanyia marekebisho.
Ushauri
huo umetolewa leo na wadau mbalimbali wa haki za binadamu katika
kongamano la kuijadili adhabu ya kifo nchini, lililoandaliwa na Kituo
cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kwa kushirikiana na Shirika la
Umoja wa Mataifa (UN).
Wadau
hao wamesema kuwa, falsafa ya ukuaji wa adhabu huzingatia vigezo viwili
ambavyo ni kutoa funzo kwa jamii pamoja ma kumrekebisha mkosaji. Wadau
hao wameitumia hoja hiyo kuisisitiza serikali kufuta adhabu ya kifo kwa
kuwa endapo mtuhumiwa akiuawa hatopata fundisho na pia kifo chake
kinatafsiriwa sawa na kosa hilo kujirudia.
Mkurugenzi
Mtendaji wa LHRC Hellen Kijo-Bisimba amesema kituo hicho hakitaacha
kuishauri serikali kuifuta adhabu hiyo kwa kuwa haisaidii kutokomeza
matukio ya mauaji na pia huenda ikaathiri watu wasio na hatia.
“Inabidi
serikali iangalie chimbuko la matukio ya mauaji ili litokomezwe na si
kuhukumu watu kwa adhabu ya kifo, hatumaanishi wasihukumiwe bali
watafutiwe adhabu nyingine kwa kuwa tangu kuanza kutumika adhabu hii
matendo ya mauaji hayajapungua,” amesema.
Ameongeza
kuwa ” Kumuua mtu si suluhisho bali kosa hilo linazidi kufanyika na si
sahihi. LHRC tunaendelea kuipinga adhabu hii sababu haisaidii kupunguza
mauaji,”
Bisimba
amedai kuwa, asilimia kubwa ya wanaohukumiwa adhabu ya kifo ni watu
wasio na kipato na kwamba hali hii huonyesha adhabu hiyo hutekelezwa
kitabaka zaidi.
Mwakilishi
wa UN, Roeland Van de Geev amesema kuwa shirika hilo halitailazimisha
serikali kuifuta sheria hiyo bali litawezesha mashirika yasiyo ya
kiserikali (NGO’s) yanayohusika na haki za binadamu nchini kuishauri
serikali kufuta adhabu hiyo.
“Nchi
zaidi ya 140 duniani zimefuta adhabu hiyo, na hakuna matukio ya kutisha
ya mauaji katika nchi husika, mfano Marekani inatekeleza adhabu ya kifo
lakini matukio ya mauaji bado yanaendelea. Hii inamaanisha kwamba
suluhu pekee ni kutibu au kuzuia vyanzo vya matukio hayo,” amesema.
Ameshauri
kuwa “Adhabu hii hafai kutekelezwa sababu inaondoa utu wa mtu. Tanzania
pamoja na nchi za Ukanda wa Afrika Mashariki zifute sheria hiyo.”
Bahame
Tom Nyanduga kutoka Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora amesema
adhabu hiyo haistahili kuendelea kutekelezwa nchini kutokana kwamba
ilianzishwa na wakoloni kwa lengo la kulinda utawala wao.
“Haki
ya binadamu ya kuishi ndiyo msingi wa haki nyingine, katiba ya 1977
inatambua haki ya kuishi. Mahakama haiwezi futa adhabu hii bali serikali
ndiyo yenye wajibu wa kuifuta sheria hiyo hivyo ni vyema ikafanya
hivyo,” amesema.
Amesema
ingawa serikali haijatekeleza adhabu hiyo kwa zaidi ya miaka 20 lakini
inawajibu wa kuifuta sababu watu wanazidi kuhukumiwa.
“Nchi
zaidi ya 20 Afrika zimefuta adhabu hii na hatusikii kama kuna kukithiri
kwa matukio ya mauaji.Ni vigumu kuhusisha adhabu ya kifo kama suluhisho
pekee la kutokomeza mauaji,” amesema.
Sheikh
Ally Hemko kutoka Baraza Kuu la Waisilamu Tanzania (Bakwata) ameshauri
jamii kuepukana na vitendo vya mauaji kwa kuwa dini hairuhusu.
“Dini
yetu hufundisha kuwa mtu anayeua nae aue ingawa pia inasisitiza kuua ni
dhambi hivyo ili kuondokana na utata huo, jamii inawajibu wa kuacha
votendo hivyo sababu hata kama sheria hiyo ikifutwa watu wasio wema
watazidi kuua,” amesema.