WACHEZAJI WA STAND UNITED 'CHAMA LA WANA' WALIA NJAA

 
LICHA ya kufanya vizuri kwenye Ligi Kuu Bara, wachezaji wa Stand United wanalia njaa kwani hawajalipwa mishahara yao ya miezi mitatu.

Stand ambayo ilianza ligi ikiwa kwenye mgogoro mkubwa wa mgawanyiko wa Asili na Kampuni, kwa sasa ipo nafasi ya pili kwenye msimamo ikiwa na pointi 16.

Akizungumza na gazeti la Habarileo juzi, kocha mkuu wa timu hiyo Mfaransa Patrick Liewig alisema wachezaji wake hawajalipwa mshahara wa miezi mitatu hivyo anaomba uongozi wa timu hiyo uwalipe.

“Miezi mitatu hawajalipwa, hawa hawahitaji kingine zaidi ya mishahara yao, viongozi wafanye wawalipe,” alisema.

" Baada ya mchezo wetu na timu ya Majimaji, uongozi ulituahidi kuwa tutapata mahitaji yetu yote lakini kwa sasa wanasema hawana pesa," alisema Liewig.

Liewig alisema kwa sasa timu yake ina hali ngumu na kwamba kwa vile wachezaji wake wanacheza kwa kujituma na uvumilivu ndio maana wanapata ushindi. Kocha huyo alilaumu mmoja wa viongozi wa benchi la ufundi kutaka kufanya hujuma ili wapoteze mechi hiyo.

" Katika mchezo wetu na Majimaji mmoja wa watu wa benchi la ufundi (anamtaja) alijaribu kuwarubuni wachezaji wetu ili tufungwe lakini wachezaji waligoma.

Wachezaji wangu wapo hapa kwa ajili ya kufanya kazi na sio kupokea rushwa. Msimu uliopita wachezaji (anawataja) walikuwa wakifanya hujuma tufungwe lakini safari hii hawapo katika timu yangu na ndio maana unaona tunakwenda vizuri,” alisema.

Kocha Liewig anamtaja mmoja wa viongozi hao wa benchi la ufundi kwamba alihusika kufanya hujuma katika moja ya mechi dhidi ya timu kubwa msimu uliopita ambapo timu yake ilifungwa mabao 4-0.

Chanzo-Habarileo
Powered by Blogger.