Ripoti mpya ya shirika la Save the Children inasema msichana wa chini ya miaka 15 huozwa kila baada ya sekunde saba duniani.
Ripoti
hiyo inasema watoto wa hadi chini ya miaka 10 wanashurutishwa kuolewa
na wanaume wazee katika nchi kama vile Afghanistan, Yemen, India na
Somalia. Save the Children wanasema ndoa za mapema zinaweza kuchangia msururu wa matatizo ambayo huathiri maisha yote ya msichana.
Mizozo, umaskini na migogoro ya kibinadamu vinatazamwa kama sababu kuu zinazowaweka wasichana hatarini ya kuozwa wakiwa bado wana umri mdogo.
"Ndoa za mapema huanzisha msururu wa matatizo ambayo humnyima msichana haki za kimsingi za kujifunza, kujikuza na kujivunia maisha yake kama mtoto," amesema afisa mkuu mtendaji wa Save the Children International Helle Thorning-Schmidt.
"Wasichana wanaoolewa wakiwa wadogo mara nyingi huwa hawawezi kuendelea na masomo, mara nyingi hudhulumiwa na waume zao, kupigwa na hata kunyanyaswa kingono. Hupachikwa mimba na pia huwa hatarini ya kuambukizwa magonjwa ya zinaa, ukiwemo Ukimwi."
Ripoti hiyo iliyopewa jina Every Last Girl, imeorodhesha nchi ambazo ni ngumu zaidi kwa wasichana baada ya kuzingatia elimu, ndoa za watoto, mimba za mapema, vifo vya wanawake wakijifungua na idadi ya wanawake bungeni.
Chad, Niger, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Mali na Somalia zinashika mkia kwenye orodha hiyo.
Shirika la Umoja wa Mataifa linalowashughulikia watoto, Unicef, linakadiria kwamba idadi ya watoto watakaoozwa wakiwa wadogo itaongezeka kutoka 700 milioni kwa sasa hadi 950 milioni kufikia 2030.
Ripoti hiyo ya Save the Children imetolewa siku ya maadhimisho ya Siku ya Msichana Duniani.