Watanzania wameungana na wenzao duniani kote kuadhimisha siku ya Afya ya Akili duniani huku Tanzania ikitajwa kuwepo kwa zaidi ya wagonjwa laki nne na nusu wanaougua maradhi hayo nchini.

Aidha mkoa wa Dar es salaam ndio unaongoza kwa kuwa na wagonjwa ambapo sababu kubwa inatajwa kuwa ni matumizi ya kupindukia ya madawa ya kulevya ikiwa ni pamoja na Bangi.
Kadhalika, mkoa wa Dodoma watu 12 wanapokelewa kila siku katika hospitali ya rufaa ya wagonjwa wa akili ya Mirembe kutokana na tatizo hilo.
Maadhimisho hayo ambayo kitaifa yamefanyika mkoani Dodoma katika hospitali ya taifa ya magonjwa ya akili Mirembe ambayo huadhimishwa kila mwaka tarehe 10 ya mwezi wa kumi.
Kauli mbiu ya maandimisho hayo ni “utu katika afya ya akili, huduma za kisaikolojia na afya ya akili kuwa huduma ya kwanza kwa wote”
Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto, Mkuu wa wilaya ya Dodoma, Christina Mndeme amewataka watanzania kuungana katika kupiga vita unyanyasaji na ukatili kwa wagonjwa wa akili na badala yake wapelekwe hospitali kwa ajili ya kupata matibabu.
Amesema tatizo la akili huathiri kufikiri,kuhisi,kutambua na kutenda na tatizo la akili kwa sasa linaongezeka ambapo  takribani watu milioni 35 wanaishi na ugonjwa huo.
Mkuu wa wilaya huyo amesema kwa mujibu wa taarifa ya akili na dawa za kulevya ya mwaka 2013/2014 za shirika la afya duniani(WHO)o mkoa unaoongoza kuwa na wagonjwa wengi ni Dar-es-salaam ambayo ina asilimia 2 ya wagonjwa ikifuatiwa na Mwanza yenye asilimia 1.2 huku mkoa wa mwisho ukiwa ni Rukwa wenye asilimia 0.2
Naye Mganga mkuu wa Mkoa wa Dodoma, DK. James Kiologwe, amesema kwa mkoa wa Dodoma wagonjwa 1256 walipatikana katika kipindi cha mwaka 2015 na kila siku wanapokea wagonjwa 12 ambao wanaugua ugonjwa huo wa akili ambao wanatoka katika maeneo mbalimbali.
Kwa upande wake, Mganga mkuu wa Hospitali ya rufaa ya wagonjwa wa akili Mirembe, Erasmus Mndeme, ameeleza sababu kuu mbili zinazosababisha ugonjwa wa akili, kuwa ni ile ya mtu kuzaliwa na vinasaba vya ugonjwa huo ambapo vinakuwa ni vya kurithi na pia inatokana na magonjwa ambayo yanashambulia kwenye ubongo ambapo mtu anaweza kuugua ugonjwa wa Maralia, uti wa mgongo na mapafu ambapo huathiri ubongo.
Amebainisha mgonjwa huyo akishatibiwa na kupona anabaki na tatizo kwenye ubongo na hivyo kupatwa na ugonjwa wa kichaa, kutokana na namna alivyoumwa.
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Bi.Christina Mndeme ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa huo akitoa hutuba ya siku ya Afya ya Akili katika tukio hilo.