Nape:Muswada wa habari kuibadili taaluma
Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Nape Moses
Nnauye akiwasilisha kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo
ya Jamii Mswada wa Sheria ya Huduma za Habari 2016 leo Mjini Dodoma
Oktoba 18,2016
SERIKALI imewasilisha mbele ya
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Jamii Muswada wa Huduma za Habari
ikieleza kuwa ni sheria itakayoleta mageuzi makubwa nchini.
Hayo yamesemwa na Waziri wa
Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Nape Moses Nnauye alipokuwa
akiwasilisha muswada wa sheria hiyo leo mjini Dodoma ambapo amesema sasa
sekta ya habari inakwenda kuwa taaluma kamili.
Waziri Nnauye amesema Sheria hii
italeta mifumo ya kisasa ya usimamizi wa sekta ya habari na mifumo
ambayo inaweza kugusa au kubadili namna wanahabari walivyozoea kutenda
au kufikirika kwa sasa lakini akasema sekta hiyo iwe tayari kwa
mabadiliko.
“Niwaombe wanatasnia wenzangu
tuwe tayari kwa mabadiliko haya ili taaluma yetu iheshimike na sisi
wenyewe tuheshimike zaidi” alisisitiza Mhe. Nnauye.
Aidha Mhe. Nnauye ametoa wito kwa wadau wote kuunga mkono muswada huo utakaojadiliwa katika Bunge lijalo la Novemba mwaka huu.
“Tuko hapa kuboresha na sio
kusuguana tukae tuiandae tasnia bora zaidi kwa kupitia na kutoa maoni
juu ya Muswaada huu wa Sheria ya Huduma za Habari 2016” alifafanua Mhe.
Nnauye.
Ameongeza kuwa kwa sasa hadi
wakati wa Bunge lijalo Serikali ipo tayari kupokea na kuyafanyia kazi
maboresho yatakayolenga kufikia maono ya muswada huu kutoka kwa wadau
ili kuipa heshima stahiki sekta ya habari.
Alisema kuwa muswada huo licha ya
huu utatatua changamoto za kutotambulika kwa sekta ya habari kama
taaluma kamili inayopaswa kuheshimiwa, pia utatatua changamoto ya
kukosekana vyombo madhubuti na huru vya usimamizi wa tasnia.
Alisema kutokana na hayo muswada unapendekeza kuundwa kwa Bodi ya Ithibati itakayoainisha sifa za mwanahabari na kuwasajili.
Aliitaja taasisi nyingine
inayoundwa kuwa ni Baraza Huru la Wanahabari ambalo litakuwa na wajibu
wa kuandaa na kusimamia maadili ya wanahabari na watawajibishana wenyewe
kwa wenyewe.
Wasomi wanena
Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa
katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dkt. Benson Bana anasema kuwa kuja
kwa sheria hiyo ni jambo la busara kwa sababu kwa sasa weledi wa
uandishi wa habari uko chini.
“Sheria hii iwe na makali zaidi
kwa wanahabari ambao watakiuka utaratibu na maadili. Hakuna nchi ambako
wanahabari wanajiendea tu bila uratibu,” alisema,
Alisema ni vyema na ni wakati
mauafaka kwa sekta ya habari kuwa taaluma kamili na kushauri kuwa
wanaoitumikia fani hiyo kwa sasa wawe tayari kwa mabadiliko.
Naye Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa
na Uhusiano wa Kimataifa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dkt William
John Walwa alisema sheria imekuja wakati muafaka na inapaswa kutatua
changamoto za fani hiyo.