MKUTANO WA ACT WAZALENDO WATOA MAAZIMIO MATATU


Chama cha ACT- Wazalendo kimemuomba Rais John Magufuli kuunda timu ya wataalamu kupitia upya rasimu ya Katiba ya Jaji Joseph Warioba na kuitisha mkutano mkuu wa kikatiba ili kuipitisha.

Chama hicho kilisema mchakato wa kura za maoni uanze upya ili kupata Katiba Mpya.


Hayo ni miongoni mwa maazimio matatu yaliyotolewa na chama hicho kwenye mkutano wa siku moja wa kidemokrasia.


Akisoma maazimio hayo, Ofisa Habari wa chama hicho, Abdallah Khamis alisema, “chama kimeazimia mchakato wa kuandika Katiba Mpya uanze kwa kufanya marekebisho ya sheria ya kura ya maoni na Sheria ya mchakato wa Katiba.”


Alisema, iwapo Serikali itaamua kwenda na Katiba Inayopendekezwa iliyopo sasa chama hicho kitaipinga kwa kufanya kampeni ya hapana kwenye kura ya maoni.


Alisema wakati mchakato wa Katiba ukiwa umesimama, Baraza la Wawakilishi Zanzibar limepitisha sheria ya kutafuta mafuta na gesi kinyume na matakwa ya Katiba ya Muungano ambayo inatambua mafuta na gesi kuwa ni masuala ya muungano.


“Mkutano Mkuu wa Kidemokrasia umeshauri kuwa chama kimwelekeze mbunge wake kuwasilisha bungeni hoja binafsi ya kufanya mabadiliko, kwa kuondoa mafuta na gesi kama jambo la muungano ili kuiwezesha Zanzibar kutafuta mafuta na gesi asilia bila vikwazo,” alisema.


Khamis alisema chama hicho kimeazimia kufanya maadhimisho ya miaka 50 ya Azimio la Arusha Februari, 2017.


“Katika maadhimisho hayo chama kifanye mkutano mkuu wa Kidemokrasia jijini Arusha na kutanguliwa na Halmashauri Kuu ya chama kwenye ukumbi uleule ambao Tanu ilifanya na kuzaa Azimio la Arusha mwaka 1967,” alisema.


Ofisa huyo alisema katika maadhimisho hayo chama kimeshauriwa kuwa wataalamu wa ndani na nje waalikwe kujadili mafanikio na changamoto za Azimio la Arusha katika miaka 25 iliyopita.

Pia, wataalamu watajadili madhara ya kutelekezwa kwa Azimio la Arusha mwaka 1992 huko Zanzibar.
Powered by Blogger.