Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam leo limetahadharisha wananchi wa Jiji hilo kuwa kuna wimbi la matapeli wanaotumia ukosefu wa ajira kama njia ya kutapeli wananchi.
Kamishna wa Kanda hiyo, Kamanda Simon Sirro amesema jeshi la polisi lilipokea taarifa kutoka kwa raia mwema ambaye alitapeliwa na watu hao.
Sirro amefafanua kuwa, matapeli hao huwarubuni watu kuwa wana kampuni zinazohusika na kutafutia watu ajira na kwamba hutoa masharti kwa anayehitaji ajira kulipia baadhi ya gharama kwa ajili ya kulipa watu wanaohusika na usaili wa kazi hizo.
Amewataka wakazi wa jiji la Dar es Salaam kuwa makini na kwa mwenye taarifa sahihi za matapeli hao kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa zao katika vituo vya polisi.
Hali kadhalika, Jeshi la Polisi limetoa onyo kwa wanaoeneza taarifa za uongo za uhalifu, ambapo wakazi wa maeneo ya Kivule, Kitunda, na Gongo la mtoto wametajwa kuongoza kwa utoaji wa taarifa hizo.
Kamanda Sirro amesema kuwa, kitendo hicho cha wananchi kutoa taarifa za uongo kinasababisha polisi kuelekeza nguvu nyingi mahala ambapo hakuna uhalifu na kuyaacha maeneo yenye uhalifu kutokana kwamba watoa taarifa hao hutoa taarifa zenye vitisho.
Amesema jeshi linafanya ufustiliaji kupitia mitandao ya simu waliyotumia wahusika ili kuwabaini na kuwachukulia hatua kali za kisheria.