MAADHIMISHO YA MIAKA 71 YA UMOJA WA MATAIFA.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga akizungumza na Waandishi wa Habari (hawapo pichani) katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam. Mhe. Balozi Dkt. Mahiga, amezungumzia umuhimu wa maadhimisho wa Siku ya Umoja wa Mataifa na faida za Jukwaa la umoja huo kwa maendeleo ya Taifa. Maadhimisho hayo yatafikia kilele tarehe 24 Oktoba, 2016.
OKTOBA 24 kila mwaka Umoja wa Mataifa hufanya maadhimisho ya kuzaliwa kwake.
Mwaka huu
mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini Tanzania kwa kushirikiana na
serikali, wadau wa maendeleo na vijana wataadhimisha miaka 71 ya uwapo
wa Umoja wa Mataifa kwa staili ya aina yake.
Kwa mujibu wa
taarifa iliyotolewa katika mkutano wa waandishi wa habari na Wizara ya
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ikishirikiana na Umoja
wa Mataifa , maadhimisho hayo mwaka huu yamelenga kuelezea kwa undani
shughuli zinazofanywa kwa pamoja kati ya pande hizo mbili ili kuwezesha
maendeleo endelevu.
Katika mkutano
huo wa pamoja, waandishi wa habari walielezwa kwa ufupi Mpango Mpya wa
Maendeleo Chini ya Ufadhili wa Umoja wa Mataifa ( UNDAP ll -2016 hadi
2021) kwa serikali ya Tanzania; na mpango wa maendeleo wa miaka mitano
wa Tanzania ambamo malengo ya maendeleo endelevu (SDGs) kama
yalivyosanifiwa na kukubalika na jumuiya ya kimataifa, yameshirikishwa.
Katika mkutano
huo na waandishi wa habari pia kulikuwepo na majadiliano ya mafanikio ya
shughuli za Umoja wa Mataifa hadi sasa duniani na pia nchini Tanzania .
Pia mazungumzo
hayo yalijikita katika malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) na umuhimu
wa malengo hayo kumilikishwa kwa wananchi na wajibu wao katika
kuhakikisha kwamba kunakuwa na utekelezaji wenye mafanikio.
Pia ilielezwa
katika mkutano huo kwamba maadhimisho ya miaka 71 ya Umoja wa Mataifa,
Siku ya Umoja wa Mataifa, yatafanyika katika viwanja vya Karimjee jijini
Dar es Salaam Oktoba 24.
Maadhimisho
hayo ambayo mwaka huu yamebeba ujumbe wa :“Uwezeshaji wa vijana Tanzania
kufikia malengo ya dunia” yanafanyika huku kukiwa na malengo mapya ya
dunia ya maendeleo endelevu.Malengo hayo ya SDGs yamelenga kuondoa
umaskini kwa kuwa na maendeleo endelevu.
Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt.
Augustine Mahiga katika mkutano na waandishi wa habari.
Aidha ujumbe
huo unaenda sanjari na mpango wa maendeleo wa awamu ya pili wa Umoja wa
Mataifa kwa Tanzania (UNDAP II) ambao unaendeleza ule wa awali wa
kuanzia 2011-16 ukiwa umejikita katika masuala ambayo ni muhimu kwenye
kukabili umaskini kwa kuwa na maendeleo endelevu.
Maadhimisho ya
mwaka huu yalitanguliwa na kongamano la vijana wapatao 200, ambao
walijadili masuala yanayogusa fursa za uchumi na maendeleo ya jamii na
mchango ambao unaoweza kutolewa na vijana kufanikisha utekelezaji wa
malengo hayo.
Maadhimisho hayo yatafikia kilele chake nchini kwa tukio litakalofanyika Visiwani Unguja Oktoba 26 mwaka huu.
Imeelezwa kuwa
maadhimisho ya mwaka huu yanaonesha uwapo wa ushirikiano mkubwa na wenye
tija kati ya Tanzania, wananchi wake na Umoja wa Mataifa.
Kaimu
Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika
la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini, Bi.Chansa Kapaya
akizungumza na waandishi wa habari.
Aidha
maadhimisho hayo yanaonesha ni kwa namna gani pande zote zipo tayari
kutekeleza mipango ya maendeleo ya Umoja wa Mataifa nchini Tanzania
yenye lengo la kusaidia utekelezaji wa malengo ya maendeleo endelevu.
Akizungumza
umuhimu wa ushirikiano huo katika kutekeleza mpango wa maendeleo wa
miaka mitano, ukiwa ni mpango wa wananchi wenyewe, Waziri wa Mambo ya
nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw Augustine Mahiga, alielezea
Tanzania kuunga mkono Umoja wa Mataifa ukifanyakazi kama taasisi moja na
kuwataka watengeneza sera kuhakikisha kwamba wananchi wote wananufaika
na ushirikiano huu wa Tanzania na Umoja wa Mataifa.
Waziri Mahiga
alisisitiza wakati Tanzania inajikita katika kutekeleza mpango wake mpya
wa taifa wa maendeleo, kuna haja ya kuhakikisha kwamba wananchi
wanaelewa na kumiliki mpango huo ambao umejumuisha malengo ya maendeleo
endelevu.
Mkurugenzi
Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Celestine Mushy (kushoto)
akifuatilia mkutano. Kulia ni Kaimu Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja
wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa
(UNDP) nchini Bi.Chansa Kapaya.
Alisema:
“Tanzania imeshirikisha malengo ya maendeleo endelevu (SDGs) katika sera
za taifa na pia katika mipango ya maendeleo inayotekelezwa katika
maeneo ya msingi yanayohitaji uangalizi kufanikisha maendeleo
endelevu”.
Hata hivyo
aliongeza kusema kwamba: “ Hiyo inajulikana wazi kwamba serikali pekee
haiwezi kufanikisha utekelezaji wa ajenda ya maendeleo endelevu bila
msaada wa sekta binafsi na wadau wetu wa maendeleo, na hivyo iko haja ya
kushirikishana. Tunaitaka sekta binafsi na wadau wetu wa maendeleo
kujiunga nasi katika juhudi hizi kwa kutuwezesha kifedha ili tuweze
kutekeleza mipango yetu ya maendeleo. Tunachohitaji sisi tunaofanyakazi
katika ushirikiano wa kimataifa kuhakikisha kwamba hatutamwacha yeyote
nyuma katika harakati zetu za kuleta maendeleo”.
Naye Mratibu wa
Mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini Bw. Alvaro Rodriguez akizungumzia
maadhimisho ya miaka 71 ya Umoja wa Mataifa na uhusiano wake alisema:
“Tanzania na Umoja wa Mataifa zimekuwa na ushirikiano wa maendeleo kwa
miongo mingi. Wakati Tanzania sasa inabadilika, msaada unaotolewa na
Umoja wa Mataifa unatakiwa kukidhi haja mpya, hasa taifa linapoelekea
katika uchumi wa kati”.
Pia katika
hotuba yake aliongeza kwamba: “Malengo ya maendeleo endelevu ni muhimu
katika ushirikiano wetu kwani unaweka umuhimu wa shughuli za Umoja wa
Mataifa nchini Tanzania za kusaidia kupatikana kwa mafanikio katika
nyanja za uchumi, ustawi wa jamii na utunzaji wa mazingira.”
(Imeandaliwa na Reginald Kisaka wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki).