Mkuu wa wilaya ya Manyoni mkoani Singida,Geoffrey Mwambe,amefuta rasmi amri yake halali yenye kumbukumbu namba AB/241/01/33  ya septemba 06 mwaka huu,iliyokuwa inatoa uhalali wa kuchangia maendeleo ya wananchi wa wilaya hiyo,ikiwemo mtu mwenye umri wa miaka 18 na kuendelea,kuchanga shilingi 15,000 kwa mwaka.

Michango mingine ni  shilingi 3,000 kwa ajili ya ushuru wa ng’ombe na punda,wakati shilingi 2,000 ni kwa ajili ya ushuru wa mbuzi na kondoo kwa mwaka.Ushuru na kodi hiyo,ni kwa ajili ya maendeleo ya wananchi.
Katika taarifa yake kwa umma na kutoa nakala kwa vyombo vya habari, Mwambe  amesema Septemba sita mwaka huu, Afisa Mtendaji wa kijiji cha Magasai tarafa ya Kintinku alifika ofisini kwake na kuomba aruhusiwe na kupatiwa amri halali ya kuwahimiza wananchi kuchangia maendeleo ya kijiji chao.
“Afisa mtendaji huyo aliwasilisha ombi hilo baada ya serikali ya kijiji kuazimia kupitia kikao cha halmashauri ya kijiji cha Magasai,waombe michango kwa wananchi.Lengo likiwa ni kusaidia na kuharakisha utekelezaji wa mipango ya maendeleo ikiwemo mradi wa ujenzi wa zahanati ya kijiji.Pia michango hiyo,itumike kumaliza uhaba wa madawati katika kijiji hicho”,alisema.
Akisisitiza,alisema lengo mahususi la uchangishaji huo lilikuwa ni kutatua kero za wana kijiji wa Magasai na kukamilisha miradi ya maendeleo, iliyopewa kipaumbele na kijiji na kuidhinishwa na kikao cha maendeleo ya kata (WDC), kulingana na miongozo ya serikali za mitaa.
Akisisitiza zaidi, Mwambe alisema amri ya aina hii (aliyotoa yeye Mwambe), ilitolewa mara ya mwisho 2013, ikiwa ni kufanikisha ombi hilo la wananchi kuchangia miradi yao ya maendeleo.
img_7632Mkuu wa wilaya ya Manyoni mkoani Singida.Geoffrey Mwambe, akiwa kwenye mikitano yake ya kuhamasisha wananchi kujileta maendeleo yao.(Picha na  Nathaniel Limu).
“Amri halali iliyotolewa na Mkuu wa wilaya ya Manyoni aliyekuwepo mwaka 2013,ndiyo iliuhuishwa na kusainiwa upya na mkuu wa wilaya ya sasa (Mwambe), Lengo ni kuipa serikali ya kijiji Magasai,nguvu ya ushawishi kuwa michango husika inatambuliwa na uongozi wa wilaya”,alisema Dc huyo na kuongeza kwa kusema;
“Ndugu waandishi wa habari,napenda kuwaeleza kuwa mafanikio ya kijiji cha Magasai katika ukusanyaji wa michango,iliwapa hamasa watendaji wa vijiji wengine kuchukua amri hii halali.Walichukua amri hiyo halali ili iweze kuwasaidia kuhamasisha michango ya maendeleo,  ambayo kwa muda mrefu baadhi ya wananchi walisita kuchangia kwa kutoamini uongozi wao”.
Mwambe alisema amefikia uamuzi wa kufuta amri hiyo halali ya septemba sita mwaka huu,kwa matarajio kuwa kwa sasa kijiji cha Magasai ambacho kililengwa,kimeisha andaa mango mkakati na madhubuti wa kuhamasisha wananchi waweze kuchangia kwa hali na mali miradi yao ya maendeleo.
Aidha,Mkuu huyo wa wilaya,ametumia nafasi hiyo,kukanusha vikali  taarifa zilizosambazwa na mitandao ya kijamii zilizohusu wananchi kuchangia maendeleo yao,kwamba zilijaa uzushi,uongo na zinafifisha juhudi za serikali na wananchi kujiletea maendeleo.
Katika hatua nyingine,mkuu huyo wa wilaya,alisema hadi sasa ujenzi wa bweni la wasichana sekondari ya Mwanzi,umechangiwa zaidi ya shilingi 9.1 milioni,na vifaa mbalimbali vyenye thamani ya zaidi ya shilingi 6.1 milioni,vimechangiwa.
“Jumla ya vifaa vya ujenzi na fedha taslimu za ujenzi wa bweni la wasichana sekondari ya Mwanzi,ni zaidi ya shilingi 15.3 milioni zinahitajika kukamilisha ujenzi huo”alisema Mwambe.
Alitumia fursa hiyo kuwasihi na kuwaomba wananchi wa wilaya ya Manyoni waishio ndani na nje ya wilaya hiyona wadau wa maendeleo mbalimbali,waendelee bila kukatishwa tama na watu wachache wenye lengo la kukwamisha maendeleo ya wilaya hiyo.