KATIBU TAWALA MKOA WA MARA AONGOZA HAFLA YA KUMU PONGEZA MKUU WA MKOA BRIGEDIA JENERALI EVANS MTAMBI.











 Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara, Ndugu Gerald Kusaya, leo tarehe 11,septemba 2026, ameongoza hafla ya kumpongeza Mkuu wa Mkoa wa Mara, Mheshimiwa Brigedia Jenerali Evans Alfred Mtambi, kufuatia kupandishwa cheo chake cha kijeshi kutoka Kanali hadi Brigedia Jenerali.

Hafla hiyo imefanyika katika viunga vya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, ikihudhuriwa na viongozi mbalimbali, watumishi wa umma, viongozi wa dini pamoja na wadau wengine wa mkoa.

Akizungumza katika hafla hiyo, Katibu Tawala Mkoa wa Mara, Ndugu Gerald Kusaya, ametoa shukrani za dhati kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuupa kipaumbele Mkoa wa Mara na kuwaamini viongozi wenye uwezo na uadilifu.

Amesema kupandishwa cheo kwa Mkuu wa Mkoa ni ishara ya kutambua weledi, uhodari, utii na utumishi wake uliotukuka katika kulitumikia taifa.

“Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuendelea kuupa kipaumbele Mkoa wa Mara. Kupandishwa cheo kwa Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa ni heshima kubwa kwetu wanaMara na ni uthibitisho wa kutambua weledi, uadilifu na ushupavu wake katika kulitumikia taifa,” amesema Ndugu Kusaya.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Mheshimiwa Brigedia Jenerali Evans Alfred Mtambi, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, kwa kumwamini na kumpa nafasi ya juu ya uongozi.

Pia amewashukuru viongozi wenzake wa Mkoa wa Mara, viongozi wa dini kwa maombi na ushirikiano wao, watumishi wa umma pamoja na wananchi wote kwa kuendelea kumuunga mkono katika kutekeleza majukumu yake.

“Ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, kwa kuniamini na kunipa nafasi hii. Nawashukuru pia viongozi wenzangu, viongozi wa dini, watumishi wa umma na wananchi wote wa Mara kwa maombi, ushirikiano na kujitoa kwao katika kulitumikia taifa,” amesema Brigedia Jenerali Mtambi.

Katika kuadhimisha hatua hiyo, Katibu Tawala Mkoa wa Mara, Ndugu Gerald Kusaya, amemkabidhi Mkuu wa Mkoa ngao ya pongezi kwa niaba ya wanaMara. Hafla hiyo pia imeambatana na zoezi la kukata keki, ikiwa ni sehemu ya kuonyesha furaha na pongezi kwa Mkuu wa Mkoa.

Powered by Blogger.