WANAWAKE, MAISHA HAYANA HISANI; TAFUTENI HELA, MILIKINI ARDHI — MMUYA
Na mwandishi wetu DODOMA
Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Kaspar Mmuya, amewataka wanawake nchini kuongeza juhudi katika shughuli za kiuchumi na kutafuta fedha ili waweze kumiliki ardhi na rasilimali nyingine kwa kujitegemea.
Mhe. Mmuya ametoa wito huo jijini Dodoma wakati akihutubia Kongamano la Kampeni ya “Linda Ardhi ya Mwanamke (Stand for Her Land)”, akisisitiza kuwa uwezeshaji wa mwanamke kiuchumi ni sehemu muhimu ya kumwezesha kutumia fursa za kisheria katika kupata na kumiliki ardhi.
Amesema takwimu zilizowasilishwa katika kongamano hilo zinaonesha kuwa asilimia 38 ya wanawake nchini ndio wanaomiliki ardhi, hali ambayo imeendelea kuhitaji jitihada za kuongeza uwezo wa wanawake kiuchumi na kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika umiliki na maamuzi kuhusu ardhi.
“Maisha hayana hisani; kila mmoja ana haki, tafuteni hela. Mambo ya kubembelezana sasa hayapo. Mfumo huu wa kiuchumi unaathiri maamuzi katika familia. Mtoto wa kike tumweke wazi kwenye mifumo yote ya kuelewa jinsi ya kutafuta fedha,” amesema Mhe. Mmuya.
Amesema uwezo wa kiuchumi huongeza sauti na nafasi ya mtu katika kufanya maamuzi muhimu ya familia na jamii, ikiwemo maamuzi kuhusu umiliki wa ardhi, akieleza kuwa elimu pekee bila uwezo wa kiuchumi inaweza isiwe na nguvu ya kutosha katika kumwezesha mtu kupata rasilimali.
Mhe. Mmuya ameitaka jamii na wazazi kuacha mtazamo wa kuwafundisha watoto wa kiume pekee kuhusu biashara na utafutaji fedha, badala yake kuwajengea watoto wa kike na wa kiume uwezo sawa wa kiuchumi tangu wakiwa wadogo.
Amesema hatua hiyo itasaidia kuongeza idadi ya wanawake wenye uwezo wa kupata na kumiliki ardhi kupitia njia zinazotambuliwa kisheria, pamoja na kutumia ardhi hiyo kama msingi wa kujenga uchumi wa familia na maendeleo yao binafsi.
Ameongeza kuwa Serikali itaendelea kuimarisha mazingira ya kisheria na kiutendaji yanayolinda haki za wanawake katika upatikanaji, umiliki na matumizi ya ardhi, huku akiwataka wanawake kufahamu haki zao na kutumia fursa zilizopo kujenga uwezo wa kiuchumi na kumiliki rasilimali kwa usalama.



