WAFANYABIASHARA WA MADUKA WAGOMEA MACHINGA KUPANGWA MBELE YA MADUKA YAO

 Wafanyabiashara wa maduka katika eneo la Mbagala Rangi Tatu, Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam, wameiomba Serikali kuingilia kati changamoto ya wafanyabiashara wadogo (Machinga) wanaofanya biashara katika maeneo ya barabara na mbele ya maduka yao, wakisema hali hiyo imekuwa ikiwazibia njia wateja, na kuziba biashara zao na kusababisha kushuka kwa mauzo.

Akizungumzia kuhusiana na  changamoto hiyo, Anafi Mohamed Selemani maarufu kama Kitonga, amesema uwepo wa wafanyabiashara hao katika maeneo ya barabarani umesababisha msongamano mkubwa wa magari na kuathiri biashara za wafanyabiashara wenye maduka, akisisitiza kuwa Serikali inapaswa kuwatafutia maeneo maalum badala ya kuwarasimisha katika maeneo ya barabara.

Amesema iwapo wafanyabiashara hao wataruhusiwa kuendelea kufanya biashara katika maeneo hayo, hasa mbele ya maduka, wafanyabiashara wanaolipa kodi na gharama mbalimbali za uendeshaji wa biashara wataendelea kupata hasara na hatimaye kulazimika kufunga biashara zao.

Kwa upande wake, Erasto Jacob Chalser, mfanyabiashara wa nguo za watoto, amesema wafanyabiashara wa maduka wamekuwa wakikabiliwa na gharama kubwa za uendeshaji, ikiwemo kodi, leseni, TRA na gharama nyingine, huku wafanyabiashara wadogo wanaofanya biashara mbele ya maduka yao wakiathiri biashara zao.

Amesema wafanyabiashara hao wanapoziba maeneo ya mbele ya maduka, wateja hushindwa kuona bidhaa zinazouzwa ndani ya maduka, hali ambayo imekuwa ikisababisha biashara zao kudorora.

Wafanyabiashara hao wameiomba Serikali kuangalia upya utaratibu wa upangaji wa machinga,








wakitaka maeneo ya mbele ya maduka yaachwe wazi ili wateja waweze kupita na kuingia kwenye maduka yao.

Wamesema licha ya kuwasilisha malalamiko yao kwa uongozi wa wafanyabiashara, bado hawajapata suluhisho la kudumu, huku wakidai kuwa machinga wamekuwa wakiondolewa na kurejea tena katika maeneo hayo.

Wafanyabiashara hao wameitaka Serikali kuhakikisha wafanyabiashara wote wanapata maeneo sahihi ya kufanyia biashara, bila kundi moja kuathiri biashara na kipato cha kundi lingine.

Powered by Blogger.