MAKIPA WAWILI WA YANGA,ROSTAND NA KAKOLANYA WAPO NJIANI KUONDOKA

WAKATI zikiwa zimesalia siku 12 tu kufika Juni 6 tarehe ambayo kipa wa Yanga Beno Kakolanya atakuwa anamaliza mkataba wake na Wanajangwani hao, taarifa zinadai kuwa Wanajeshi wa JKT Tanzania wametega ‘mabomu’ wakisubiri kubutua kwani wanaamini yeye ndiye kipa muafaka kwa ajili ya msimu ujao.
  
Taarifa za ndani  kutoka kwa maafande hao zinadai kuwa wanajiandaa kumalizana na kipa huyo siku yoyote.
Chanzo chetu madhubuti kwenye masuala ya usajili kimepasha kuwa JKT wamekuwa wakimhitaji Kakolanya kwa muda mrefu lakini walikuwa wakisubiri hatma yake klabuni hapo ambapo kitendo cha kipa huyo kuwa hajafanya mazungumzo yoyote ya mkataba mpya hadi sasa kimewapa nguvu kwamba wanaweza kuingia ‘vitani’.

Kakolanya alipoulizwa kuhusu taarifa hizo  hakuwa tayari kuthibitisha au kukataa huku akisisitiza kila kitu kitafahamika mara atakapomaliza mkataba wake.

 “Mimi bado mchezaji wa Yanga bwana kwahiyo siwezi kuzungumzia ishu ya timu nyingine, vumilieni kidogo siku chache nimalize mkataba halafu kila kitu kuhusu mimi kitafahamika. Sijajua viongozi wangu wana mpango gani lakini ni kweli mkataba umebaki siku 12,” alisema Kakolanya.

kwa upande mwingine  maisha ya Youthe Rostand ndani ya yanga  ni kama vile yamefikia ukomo kwani ‘wanene’ wa kamati ya usajili ya klabu hiyo hawajaridhishwa na kiwango chake msimu huu hivyo wanataka kuachana nae.

Kama Yanga itaachana na Rostand huku pia ikimkosa Kakolanya inamaanisha ni kipa kinda Ramadhan Kabwili pekee ndiye atakayebakia kikosini hapo jambo ambalo litawalazimu kusajili makipa wengine.
Powered by Blogger.