BITEKO AUNGA MKONO AGIZO LA WAZIRI MKUU KWA VITENDO, ACHANGIA MABATI 100 KUPAUA SHULE YA SEKONDARI AZIMIO
Mbunge
wa Jimbo la Bukombe Mkoani Geita ambaye ni Naibu Waziri wa Madini Mhe
Doto Mashaka Biteko akihutubia mamia ya wananchi katika Kijiji cha Kilimahewa kilichopo katika kata ya Bulangwa wakati wa ziara za kijimbo hivi karibuni. Picha Zote Na Mathias Canal.
Baadhi ya wananchi katika Kijiji cha Kilimahewa kilichopo katika kata ya Bulangwa wakifatilia hotuba ya Mbunge wa Jimbo la Bukombe Mkoani Geita ambaye ni Naibu Waziri wa Madini Mhe Doto Mashaka Biteko wakati wa ziara za kijimbo hivi karibuni.
Na Mathias Canal, Bukombe-Geita
Mbunge
wa Jimbo la Bukombe Mkoani Geita ambaye ni Naibu Waziri wa Madini Mhe
Doto Mashaka Biteko ameendelea kutekeleza agizo la WaziriMkuu
Mhe Kassim Majaliwa alilolitoa 2 Aprili 2018 wakati wa dhifa ya
uzinduzi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2018 katika uwanja wa
Magogo mkoani Geita Katika sherehe hizo zilizonakshiwa na Kaulimbiu ya
mbio za mwenge kwa mwaka huu ambayo ni ‘Elimu ni ufunguo wa maisha,
wekeza sasa kwa maendeleo ya Taifa letu.’
Waziri
Mkuu aliwagiza viongozi wa mikoa ya Tabora, Geita, Mtwara na Shinyanga
ambayo inaongoza kwa utoro wa wanafunzi kwa shule za msingi na kwa
sekondari wahamasishe umuhimu wa elimu na mahudhurio endelevu shuleni kwani miongoni mwa sababu zinazopelekea wanafunzi kutoelimika ipasavyo ni pamoja na utoro shuleni.
Kupitia agizo hilo Mhe Biteko amechangia
mabati 100 geji 28 yenye thamani ya Sh 2.6 milioni kwa ajili ya
ukamilishaji wa kupaua vyumba vya madarasa katika shule ya sekondari
Azimio Wilayani Bukombe ikiwa ni sehemu ya hamasa kwa wanafunzi kuwa na
maeneo bora ya kusomea.
Mara
baada ya uzinduzi wa Mwenge huo wa Uhuru 2 Aprili 2018 kabla ya
kuelekea Mjini Dodoma kwa ajili ya shughuli za Bunge zilizoanza 3 Aprili
2018 Mhe Doto Biteko alizuru Kijiji cha Nampalahala kilichopo Kata ya
Busonzo na kujionea jinsi ujenzi wa maabara unavyoendelea ambapo pia
alichangia matofali
10,000 kwa ajili ya ukamilishaji Wa vyumba vya maabara ili kurahisisha
uanzishaji wa shule ya sekondari wa Kata ya Busonzo wilayani Bukombe.
Akihutubia mamia ya wananchi waliojitokeza juzi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Kilimahewa kilichopo katika kata ya Bulangwa, Mhe Biteko alisema kuwa Serikali ya awamu ya tano inyoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli, imedhamiria kuboresha elimu katika ngazi zote nchini, kuanzia Elimu ya Awali hadi Elimu ya Juu hivyo wananchi wanapaswa kuitumia fursa hiyo kwa maendeleo ya wilaya hiyo na Taifa kwa ujumla.
Alisisitiza
kuwa serikali imeweka mkakati wa kutoa elimu bure kwa wanafunzi wote
nchini kuanzia ngazi ya msingi hadi sekondari hivyo jukumu la wazazi ni
kuwapeleka watoto shule ili kunufaika na matunda ya serikali katika
utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya mwaja 2015-2020.
Aliongeza
kuwa wananchi wanapaswa kukiunga mkono Chama Cha Mapinduzi kwani ndicho
chama pekee nchini kinachoshughulika na matatizo ya wananchi ikiwemo
kuboresha shughuli mbalimbali za maendeleo katika kuboresha elimu, afya,
miundombinu na huduma zingine zikiwemo upatikanaji wa maji.
MWISHO.