MKUU WA MKOA WA MARA ADAMU MALIMA AWATAKA WANANCHI KUTOA USHIRIKIANO ZOEZI LA UCHUKUAJI TAKWIMU.

WANANCHI mkoani Mara wametakiwa kushiriki kikamilifu katika zoezi la utafiti wa mapato na matumizi ya kaya Binafsi linaloendelea nchini kwa kutoa taarifa sahihi kwa wakati ili kuwezesha serikali kupata takwimu rasmi zitakazotumika kupanga na kutekeleza miradi ya maendeleo.
Mwito huo umetolewa jana na mkuu wa mkoa huo Adam Malima alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake ambapo alisema utafiti huo utasaidia kuweka msingi katika kutambua viashiria vya kiuchumi, ajira na ustawi wa jamii ili kupata makadirio ya jumla ya mwendo wa matumizi ya kaya na kuandaa fahirisi za bei.
“Taarifa zinazokusanywa kutoka katika kaya pamoja na wanakaya zitatunzwa kwa usiri mkubwa kama inavyotakiwa kwa mujibu wa sheria ya Takwimu namba 9 ya mwaka 2015 na hazitakiwi kuonekana kwa mtu yeyote asiyehusika na ufafiti huu,pia taarifa za kaya zote zitajumuishwa kwa pamoja na kuwekwa katika mchakato wa kuandaa ripoti ya kitakwimu”alisema Malima.
Alisema utafiti huo wa mwaka 2017/18 unahitaji sana ushirikiano kutoka kwa wananchi wote hususan katika kaya zile ambazo zimechaguliwa kitaalamu kuwakilisha sampuli za kaya zilizopo mkoani hapa, kwakuwa utafiti utatoa makadirio ya uchumi jumla hasa matumizi ya kaya kwa ajili ya takwimu za pato la Taifa(Gross Domestic Product-GDP).
Kwa upande wake Meneja wa Takwimu Mkoani hapa Ramadhani Mbega alisema utafiti ulianza kutekelezwa Desemba mwaka 2017 na unatarajia kukamilika Novemba mwaka huu ambapo kila kaya iliyochaguliwa itahojiwa kwa siku 14 mfulilizo hatua inayofanyika baada ya mdadisi kukubaliana na mkuu wa kaya husika.
Mbega alisema utafiti huu umedhamiria kutoa takwimu za hali ya umaskini na takwimu nyingine ili kusaidia serikali na wadau wengine kutathmini hatua zilizofikiwa katika kutimiza malengo mbalimbali ya kitaifa na kimataifa yakiwemo yaliyoainishwa katika mpango wa pili wa Taifa wa Maendeleo wa miaka Mitano(2016/17-2020/21) na Malengo ya Maendeleo Endelevu.
“Utafiti unatarajia kukusanya taarifa kutoka kaya binafsi kwenye kata zipatazo 34 za mkoa huu zinazohusu kaya na wanakaya,uzazi na unyonyeshaji,elimu,afya,uraia, uhamiaji,ulemavu,bima, hali ya ajira biashara na mapato ya kaya na makazi ya kaya taarifa zingine ni matumizi ya nishati, huduma ya maji safi na maji taka,utalii wa ndani, uwekezaji wa kaya nakadhalika”alisema.
Mwisho.