Kocha mpya Simba asema hamjui Omog ila ‘kitaeleweka’ tu

Kocha Masoud alipowasili Airport, Dar
KOCHA Masoud Juma wa Rayon Sports ya Rwanda ametua nchini muda mfupi uliopita kumalizana na Wekundu wa Msimbazi, Simba ili akabidhiwe mikoba iliyoachwa na Jackson Mayanja aliyejiuzulu hapo jana.
Kocha huyo mtanashati raia wa Burundi atatambulishwa mbele ya wanahabari muda mfupi ujao makao makuu ya klabu hiyo mtaa wa Msimbazi na baada ya hapo ataungana na kocha mkuu Joseph Omog kwenye maandalizi ya mchezo dhidi ya Njombe Mji.
Mara baada ya kuthibitika kuwa yeye ndiye mrithi wa Mayanja Blog hii ilimtafuta kwa ajili ya kufanya nae mahojiano ndipo alipoweka wazi kuwa anakuja nchini kuwa msaidizi wa Omog ambaye hamfahamu kabisa.
“Simfahamu kabisa Omog, tutafahamiana nikija huko, ila hilo lisiwape hofu, tutafanya kazi vizuri kwa maana mpira ni ule ule na lugha yake ni ile ile,” alisema Masoud.
Akiizungumzia klabu ya Simba Masoud alisema “sijawahi kuingia uwanjani kuitazama ikicheza, lakini nakumbuka nilicheza nayo fainali ya CECAFA nikiwa nahodha wa Prince Louis ya Burundi.”
Mayanja alitangaza kujiuzulu kuifundisha timu hiyo kwa kile kilichoelezwa kuwa ni matatizo ya kifamilia yanayomlazimisha kurejea nchini kwao Uganda.