TUNDU LISSU: SIPENDI KUKAMATWA MAANA MAHABUSU SI PAZURI ILA SITAACHA KUPAZA SAUTI



Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu amesema hapendi kukamatwa na vyombo vya dola kwa kuwa mahabusu si mahala pazuri pa kuishi watu hususan wasiokuwa na hatia, hata hivyo amesema kitendo hicho hakitamuogofya na kuzuia harakati zake za kupaza sauti.


Lissu ameyasema hayo jana jijini Dar es Salaam, wakati akizungumza na wanahabari kuhusu matukio ya baadhi ya viongozi na wafuasi wa Chadema kukamatwa na vyombo vya dola, na kuwekwa mahabusu.


“Mimi sipendi kukamatwa, niwaambie mahabusu si mahala pazuri pa kwenda, hasa ukiwa huna kosa, inafika mahali inabidi uamue.

“Nipige magoti na kupelekwa machinjioni kama mwanakondoo mtiifu au nipelekwe machinjioni nikiwa napiga kelele dunia nzima isikie? Sitanyamaza na wenzangu hawatanyamaza,” alisema Lissu.

Alisema wapinzani wataongea na kufanya kile wanachopaswa kwa mujibu wa katiba na sheria na si kunyamaza kwa sababu ya mtu.

“Tutafanya kile tunachotakiwa kufanya, tutasema yanayohitajika, kama kuna mtu anafikiria wajibu wake kutukataza tusiseme ama tukisema tuadhibiwe na yeye atimize wajibu wake,” alisema Lissu.


Lissu ambaye mpaka sasa ana kesi za jinai takribani nne katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, ikiwemo ya uchochezi, amedai kuwa baadhi ya viongozi na watumishi wa umma wako katika hali ya hofu katika utendaji kazi wao, huku akiwataka wananchi kupaza sauti ili hali hiyo iondolewe.


“Hofu kila mahali, mahakamani na hata kwenye utumishi wa umma hakuna aliyeko salama. Viongozi wa dini wako kimya wanadhani wako salama. Tunahitaji kupaza sauti kila mmoja kwa nafasi yake,” alisema.
Powered by Blogger.