JELA MIAKA 30 KWA KUBAKA NA KUMPATIA UJAUZITO WANAFUNZI.;

Na COSTANTINE MATHIAS, Maswa.
MAHAKAMA ya wilaya ya Maswa mkoa wa Simiyu imemhukumu Elisha Edward (30)kazi wa kijiji cha Muhida wilayani humo kwenda jela miaka 30 jela baada ya kupatikana na hatia ya kumbaka Mwanafunzi na kumsababishia ujauzito.

Hukumu hiyo imetolewa jana na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo,Fredrick Lukuna  baada ya kuridhika bila shaka na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo na upande wa mashitaka.

Akitoa hukumu hiyo hakimu huyo alisema kuwa anatoa adhabu hiyo ili liwe fundisho kwa watu wengine wenye nia  mbaya ya kutaka kutenda kosa kama hilo katika jamii.

Awali ilidaiwa mahakamani hapo na Mwendesha Mashitaka, Mkaguzi wa Polisi,Nassibu Swedy kuwa mshitakiwa alitenda kosa hilo mwezi April mwaka jana majira ya saa 11.00 jioni.

Mwendesha mashitaka aliieleza mahakama hiyo kuwa mshitakiwa alimbaka mwanafunzi huyo wa kike(jina linahifadhiwa) mwenye umri wa miaka 14 ambaye alikuwa ni mwanafunzi wa darasa la Sita katika shule ya msingi Muhida.

Alisema kuwa kosa hilo ni kinyume na kifungu cha 130 (1) (2) (e) na kifungu 131(1) vifungu vya  sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 marejeo ya mwaka 2002.

Mkaguzi Nassibu alisema kuwa katika kumbaka huko mshitakiwa alimsababishia ujauzito mwanafunzi huyo  na hivyo kumfanya kutoendelea na masomo  na hivyo kuiomba mahakama kutoa adhabu kali kwa mshitakiwa ili liwe fundisho kwa watu wengine wenye nia ya kutenda kosa kama hilo..
Powered by Blogger.