DAWA ZA KINGA TIBA KUANZA KUTOLEWA KWA WANAFUNZI WA SHULE ZA MSINGI KUANZIA JULY. 18. MKOANI MARA;
Na makaliblog; musoma.
WANANCHI mkoani Mara wametakiwa kutowazuia watoto wao kwenda shule ifikapo julai18 mwaka huu ili kutoepuka kumeza dawa kinga tiba dhidi ya magonjwa ya kichocho na minyoo ya tumbo kwasababu hazina madhara kwa mtumiaji.
Kauli hiyo ilitolewa jana na mkuu wa mkoa huo Charles Mlingwa alipokuwa anafanya uzinduzi wa mpango wa Taifa wa kudhibiti magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele(NTDCP) lakini yana athari kubwa kwa binadamu.
‘’Dawa hizi ni salama kwa mujibu wa shirika la afya duniani (WHO), wizara ya afya maendeleo ya jamii jinsia wazee na watoto,lakini kwa mujibu wa mamlaka ya chakula na dawa(TFDA) kwa hali hiyo wananchi wa mkoa wa Mara hawana sababu ya kuwa na dhana potofu juu ya umezaji dawa hizo kwa watoto wao’’alisema Mlingwa
Alisema hakuna serikali yoyote duniani ambayo iko tayari kuwaangamiza wananchi wake kwa kuwapa dawa au vyakula vyenye madhara katika afya zao kwa kuzingatia hilo ameitaka jamii kutowazuia watoto kufika shule julai 18 kwasababu ndio siku pekee iliyotengwa kwa ajili ya kutoa dawa hizo kwa wanafuzi wa shule za msingi.
Pia alitoa wito kwa wazazi, walezi kushirikiana na walimu pamoja na kamati za shule ili kuandaa mazingira bora ambayo kutakuwa na chakula ili watoto waweze kula na kushiba kabla ya kumeza dawa hizo ili kuepuka maudhi madogomadogo yanayosabashwa na dawa hizo.
Kwa upande wake Afisa mpango huo nchini Ambakisye Mhiche alisema mpango ulianza mwaka 2016 huku magonjwa matano yanayoshughulikiwa chini ya mpango aliyataja kuwa ni usubi,vikope kichocho,monyoo ya tumbo,matende na mabusha huku wadau wanaosaidia mpango huu wametoa sh.milioni 203 ili kusaidia mkoa kutekeleza majukumu hayo.
Alisema kwa mujibu wa utafiti waliofanya mkoa wa Mara unaathiriwa na magonjwa makuu mawili ambayo ni magonjwa ya kichocho na minyoo ya tumbo ambapo magonjwa haya yanaathiri sana mikoa ya kanda ya ziwa kwa maana ya Mwanza,Mara,Kagera,Shinyanga,Simiyu pamoja na mkoa wa Kigoma.
‘’Tunatoa dawa hizi kinga tiba kwa watoto wenye umri wa miaka 5 hadi 15 kwa walioko shule za msingi na ambao hawapo shuleni kwasababu tulifanya tafiti tukachukua kinyesi,mkojo na damu kutokana na majibu tuliyopata ndio tukaona tuje na mpango huu wa kuwasaidia watoto pamoja na kuwaeleza wazingatie usafi lakini bado tunashindwa kuwadhibiti tunataka asiathirike zaidi hizi dawa zinawaponya waliathirika’’alisema.
Naye Mganga mkuu wa mkoa huo Francis Mwanisi alisema jumla ya shule 833 za serikali na binafsi zitafikiwa na mpango huo ambapo alitaja idadi ya walengwa kuwa ni watoto laki 588,029 huku mradi huo unadhaminiwa na shirika la uingereza la DFID(Depertment For International Development) ambapo unasimamiwa na wizara ya afya maendeleo ya jamii jinsia wazee na watoto.