Zitto Kabwe Afunguka Mazito kutimuliwa kazi kwa Mkurugenzi Mkuu wa EWURA
Hili la Mkurugenzi Mkuu wa EWURA linahusu tangazo la leseni ya Kampuni ya kifisadi ya IPTL?
Ni
muhimu sana Rais afahamu kwamba kuna kazi kubwa ya chinichini inafanywa
na wasaidizi wake ( sina hakika kama yeye Rais anajua na au ameruhusu
kazi hiyo ) kuendeleza wizi huu wa watu wa PAP ya Harbinder Singh Seth
na IPTL.
Kwenye
kesi ya Standard Chartered Bank dhidi ya TANESCO huko mahakama ya ICSID
ambapo TANESCO wanatakiwa kulipa shilingi 352 bilioni kwa Benki hiyo,
Wanasheria wa TANESCO na wale wa PAP/IPTL wanashirikiana kwa karibu mno.
Kwenye rufaa, TANESCO wametakiwa waweke fedha hizo kwanza kwenye
akaunti ya Benki ya nje kabla ya rufaa kusikilizwa.
PAP/IPTL
wanalinda ufisadi wao kwa kujifanya wanashirikiana na TANESCO kwenye
kesi. Kwenye Taarifa ya PAC kuhusu Tegeta Escrow Account, tuliweka wazi
kuwa PAP/IPTL waliweka dhamana kuwa ikitokea madai yeyote yale dhidi ya
TANESCO basi PAP/IPTL italipa.
Madai
yametokea, matapeli hawa wanajifanya kushirikiana na Shirika letu na
Wanasheria wa Serikali wanawasaidia matapeli hawa na sasa wanataka
kuwaongezea leseni ya Biashara. Kwanini Serikali isitumie ile Indemnity
kuwataka PAP kulipa hizi fedha? Kwanini Serikali inayosema inapambana na
ufisadi inawakumbatia mafisadi wa PAP/IPTL?
Kwanini
Serikali iliyoonyesha ujasiri wa kupambana na Kampuni kubwa kama
Acacia/Barrick inayumbishwa na matapeli hawa? Tena tapeli mmoja tu
Harbinder Singh Seth?
Vyombo
vya Serikali pia vinahusika na kuwalinda hawa matapeli. Kwa mfano, huko
ICSID Shirika letu la TANESCO kupitia wanasheria wake wamepeleka hoja
kwamba Maazimio ya Bunge kuhusu Tegeta Escrow hayana msingi wowote wa
kisheria na kwamba Bunge linapiga porojo tu.
Wanasheria
hawa wameomba Ofisi ya Bunge iwape barua kuthibitisha kuwa Maamuzi ya
bunge hayana msingi wowote na ni maoni tu yanaweza kudharauliwa na
kutupiliwa mbali. Shirika la Umma linalosimamiwa na Bunge linapeleka
barua kwenye vyombo vya kibeberu kuwa Bunge porojo tupu.
Pia
kwa kudanganywa na PAP/IPTL, TANESCO wamepeleka madai kuwa PAC
ilihongwa kufikia maamuzi yaliyofikiwa na Bunge. Wametengeneza barua
pepe za kujaribu kushawishi madai yao hayo na hata Taasisi muhimu kama
PCCB waliingia kwenye mkenge huo na kuniita kunihoji.
Niliwapa
ushirikiano wote na kuwapa simu na computer zangu wachunguze barua pepe
zile za kuchonga wakakuta hakuna lolote. Sikuwaacha, niliwaambia kuwa
wao ni mawakala wa mashetani.
Wanashirikiana
na matapeli kuwaibia Watanzania. Idara ya Usalama wa Taifa, inahusika
moja kwa moja na kazi hii inayofanywa na PAP/IPTL ili kufanikisha mradi
huu wa kitapeli. Sina hakika kama Rais aliidhinisha haya maana TISS na
PCCB wanawajibika kwa Rais moja kwa moja.
Hivyo,
inawezekana kabisa mpango wa kuongeza leseni ya IPTL akawajibishwa mtu
wa EWURA kwa sababu ndiye alitoa tangazo la leseni, lakini huyo mtu wa
EWURA anaweza kuwa ameshinikizwa na watu wa Usalama wa Taifa kufanya
hivyo. Mimi naamini Rais, kwa jinsi alivyo, hawezi kuwa anahusika na
haya matapeli, lakini Rais mtumbuaji anakaaje miezi 20 kwenye Kiti za
Enzi bila kumaliza suala la IPTL ilhali kuna Maazimio ya Bunge
yanayopaswa kutekelezwa?
Nawapa
kazi ndogo Watanzania, tazameni lile Tangazo la EWURA kuhusu IPTL
nililowawekea hapa siku limetoka. Tazameni umiliki na wamiliki wa IPTL
hivi sasa. Kuna hisa 16% kwa kampuni mbili zenye majina ya ujanja
ujanja. Kina nani hao wamegawiwa hizo hisa tena wakati wa Uongozi wa
Rais John Pombe Magufuli.