MWENYEKITI WA KIJIJI ATEKWA IKWIRIRI MWINGINE AOKOTWA MTONI;
Mwenyekiti
wa Serikali ya Kijiji cha Kati, Ikwiriri, Athuman Mtoteka anadaiwa
kutekwa na watu wasiojulikana akiwa nyumbani kwake.
Mwenyekiti huyo ambaye anawakilisha chama cha Wananchi CUF, anadaiwa kutekwa jana kati ya saa moja na mbili usiku.
Akithibitisha
kutokea kwa tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Onesmo Lyanga
amesema watu wasiojulikana walifika nyumbani kwake kwa miguu kisha
kumchukua na kwenda naye kusikojulikana.
Amesema taarifa za tukio hilo zilitolewa katika kituo cha Polisi Ikwiriri leo Alhamisi asubuhi na mkewe.
Lyanga
ameeleza kuwa baada ya kutolewa kwa taarifa hizo kituoni hapo, Polisi
tayari wamefungua jalada la uchunguzi dhidi ya tukio hilo.
"Tumepokea
taarifa hizo toka kwa mkewe akielezea mumewe kuchukuliwa na watu
wasiojulikana na kuondokanae kusikojulikana" amesema Lyanga.
Kadhalika
taarifa toka kwa majirani wa mwenyekiti huyo zinaeleza kuwa waliwaona
watu watano waliofika nyumbani hapo wakitembea kwa miguu kisha kumkamata
na kuondoka naye.
Katika
tukio jingine, maiti ya mtu mmoja ambaye hajatambulika jina lake
imekutwa ikielea ndani ya Mto Rufiji, Kitongoji cha Ngwalo kilichopo
katika Kijiji cha Mtunda A, wilayani Kibiti.
Kamanda
Lyanga amesema uchunguzi wa daktari juu ya maiti hiyo ulionyesha
marehemu alikuwa na jeraha moja kichwani lililotokana na kupigwa risasi.
Lyanga
amesema marehemu alikuwa amefungwa kamba katika mikono yake yote na
maiti hiyo ilikuwa imeanza kuharibika kutokana na kukaa majini kwa
muda mrefu.
Amesema kutokana na maiti hiyo kuanza kuharibika waliuruhusu uongozi wa kijiji hicho kuizika jana Jumatano.
Amesema
baadhi ya wananchi wa kijiji hicho waliiona maiti hiyo ikielea majini
kwenye mikondo ya maji ya Mto Rufiji kisha kutoa taarifa kwa uongozi wa
kijiji hicho nao waliotoa taarifa Polisi.
Kutokana
na matukio hayo, Jeshi la Polisi mkoani Pwani kupitia kwa Kamanda wa
Polisi wa Mkoa, Onesmo Lyanga limetoa wito kwa wananchi waishio katika
wilaya za Kibiti na Rufiji kuchukua tahadhari dhidi ya vitendo vya
mauaji yanayozidi kutokea katika wilaya hizi mara kwa mara.
