KANISA LA advetist KAMUNYONGE MUSOMA WASHIRIKI KUWAOMBEA WANAFUNZI WA LUCK VICENT WALIOPARTA AJALI

Serikali mkoani Mara imeyahakikishia
madhehebu mbalimbali ya kidini kwamba itaendelea kushirikiana nayo kutokana na
mchango wake mkubwa katika kudumisha amani na umoja wa Watanzania ulioasisiwa
katika taifa hili na Baba wa Taifa Marehemu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Kauli hiyo imetolewa hapo Mei 20
mwaka huu na Mkuu wa mkoa wa Mara Dk Charles Mlingwa wakati alipowaongoza
maelfu ya waumini wa Kanisa Kuu la Waadventista Wasabato (SDA) la Kamunyonge
lililopo mjini Musoma katika ibada maalum ya kuwaombea majeruhi wa ajali ya
wanafunzi iliyotokea wilayani Karatu mkoani Arusha Mei 6 mwaka huu.
Dk Mlingwa katika hotuba yake iliyosomwa
kwa niaba yake na Katibu Tawala wa wilaya ya Musoma Justine Manko amesema
madhehebu ya dini yameendelea kutoa mchango mkubwa wa kudumisha
amani,upendo,umoja na mshikamano miongoni mwa Watanzania huku pia yakileta
maendeleo kwa wananchi kupitia huduma mbalimbali katika sekta za
Afya,Elimu,Maji na Uchumi.
Amesema ni kwa msingi huo serikali ya
awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dk John Magufuli imeendelea kushirikiana na
madhehebu hayo ya kidini katika kuhakikisha kwamba wananchi wanafanya kazi zao
za kimaendeleo kutokana na amani iliyodumu hapa nchini baada ya kuasisiwa kwake
na marehemu Mwalimu Nyerere tangu nchi ilipopata uhuru wake hapo Desemba 9 mwaka
1961.
Kwa upande wake Mchungaji wa kanisa hilo
la Waadventista Wasabato toka mkoani Dodoma David Mbaga aliyeendesha ibada hiyo
maalum, alimuomba Mwenyezi Mungu kuleta uponyaji kwa majeruhi kupitia kwa madaktari
wa Hospitali ya Mercy iliyopo Jiji la Sioux, IOWA nchini Marekani ambapo
wanaofanya matibabu ya kina ya mifupa kutokana na majeraha waliyopata ikiwamo
kuvunjika mifupa ya miguu, mkono, taya, shingo na nyonga.
Mchungaji Mbaga ambaye pia aliendesha
semina ya wiki moja ya watu kumjua Mungu sambamba na elimu ya ujasiriamali
katika kanisa hilo Kuu la SDA la Kamunyonge tangu Mei 14 hadi Mei 20 mwaka huu,
alisema ajali hiyo ya wanafunzi wa shule ya Msingi Lucky Vincent iliyoua watu
35, imeleta majonzi makubwa kwa familia,ndugu na jamaa za marehemu waliopoteza
maisha katika ajali hiyo.
Ibada hiyo pia ilihudhuriwa na wageni
mbalimbali akiwemo Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Musoma
Daudi Misango, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Musoma
(MUWASA) Said Gantala, viongozi na waumini wa madhehebu mbalimbali ya kidini
wakiwemo wachungaji.