AJIRA ZA MUDA TASAF ZAPUNGUZA ADHA YA MAJI ITILIMA.
Na Costantin mathias.SIMIYU.
Wanufaika wa ajira zamuda toka TASAF III wakiaonyesha moja ya visima walivyochimba kwa nguvu zao.
Wananchi Wilayani Itilima mkoani
Simiyu wameanza kunufaika na mpango wa kunusuru kaya masikini (TASAF III)
kupitia ajira za muda ambapo wameweza kuibua miradi ya kujiletea maendeleo kwa
kujenga visima vya maji na Mabwawa.
Aidha ajira hizo za muda zilikuwa
zikiwanufaisha walengwa wa TASAF kwa kulipwa ujira pindi wanapofanyakazi katika
miradi hiyo waliyoiibua wenyewe kama kipaumbele katika maeneo yao.
Hayo yalibainishwa na Mhandisi wa
maji wa Wilaya hiyo Godluck Masige, mbele wadau wa maendeleo wanaofadhili
mpango huo waliofika wilayani humo kukagua utekelezaji wa ajira za muda kwa
wanufaika hao.
“ wananchi waliibua vipaumbele
vyao na Mpango ulikuwa ukitoa fedha kwa ajili ya kuvitengeneza visima hivyo ili
viwe bora zaidi na salama, walioshirikia kuchimba walilipwa kupitia mpango
ambao pia walikuwa ni walengwa, sasa hivi visima vyote vinatoa maji” alisema
Masige.
Masige aliongeza kuwa Serikali
Wilayani humo imeweka mpango wa kuviwekea pampu visima vyote 194 vilivyochimbwa
kupitia mradi wa TASAF ili kuwarahisishia wananchi kupata maji kwa urahisi
zaidi kuliko teknojia inayotumika sasa ya kuvuta maji kwa kamba.
Alisema kuwa mbali na visima
hivyo vijiji vingine wamechimba mabwawa ambayo yameanza kutumika na wananchi
wenyewe ndiyo waliopewa fursa ya kuchagua mradi kama kipaumbele kikuu kwao.
Wanufaika wa TASAF III wameshukuru kwa
kutatuliwa changamoto ya upungufu wa maji kwa mpango huo kwa kutoa ajira za
muda katika uchimbaji wa visima vya maji na kuomba kuongezewa idadi ya visima
hivyo katika awamu nyingine ya utekelezaji wa mradi ili waweze kuondokana na
adha ya ukosefu wa maji
“Tunaishukuru sana TASAF kutuletea
maji kwa visima hivi kupitia ajira za muda, tulikuwa tunatembea muda mrefu sana
zaidi ya saa moja kufuata maji, lakini sasa hivi maji yapo karibu tena ni maji
safi na salama” amesema Lubili Noni mkazi wa Migato.
Kilolo Magige na Mahila Limbu ni
wananchi walionufaika na miradi hiyo, wanaeleza kuwa wamekuwa wakihangaika
kutafuta maji ambapo mpango huo umewawezesha kuondokana na changamoto hiyo.
Kwa upande wake Dampo Ndenzako
kutoka shirika la kazi Duniani, ajira za muda na hifadhi ya jamii, alishauri
serikali kuendeleza miradi ambayo inatekelezwa na TASAF hasa inayoibuliwa na
wananchi kupitia ajira za muda.
Alisema kuwa kuwepo kwa mabwawa
yatasaidia kuongeza fursa ya kilimo kwa wananchi kwa kuanzisha kilimo cha
umwagiliaji na kupata fedha za ziada.
‘’mipango ya TASAF lazima pawepo na
ushirikiano toka ngazi za serikali na wataalamu ili waweze kuwatembelea
wananchi hawa pindi wanapoibua miradi ili iwez kuwa endelevu’’ alisema
Ndenzako.
Wilaya Itilima ni moja ya Wilaya
tano zinazofanyiwa tathmini ya utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru kaya Maskini
(TASAF III) katika awamu hii, tathmini inayofanywa na wataalam kutoka TASAF
Makao Makuu, Benki ya Dunia na wadau wengine wa maendeleo (wadau washiriki wa
mradi) ambao ni UNDP, UNFPA, ILO pamoja na Umoja wa Nchi za Ulaya(EU).
Kibao cha Mradi wa Maji cha TASAF.
NA. MAKALIBLOG.