NAMNA MKUTANO WA CUF ULIVYO VAMIWA NA MAKANJANJA
VURUGU
kubwa zimetokea katika mkutano wa viongozi wa Chama cha Wananchi (CUF)
Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam baada ya kuvamiwa na genge la watu
wanane waliokuwa na silaha za moto.
Watu hao waliingia ndani ya chumba cha mkutano huo na kuwapiga viongozi wa CUF na waandishi wa habari.
Tukio
hilo lilitokea jana saa 5:10 asubuhi katika Hoteli ya Niva iliyopo
Mabibo, wakati Mwenyekiti wa CUF Wilaya ya Kinondoni, Juma Nkumbi,
alipokuwa akielezea matukio yanayoendelea wilayani kwake, huku akidai
kuwa ni kinyume na katiba ya chama hicho.
Akiwa
katikati ya mkutano huo, ghafla waliingia watu wanane wakiwa wameziba
nyuso kwa vitambaa usoni na walivamia meza kuu waliyokuwa wamekaa
viongozi hao na kuanza kuwashambulia kwa mapanga na mikanda, huku mmoja
wao akiwanyooshea bastola.
Hata
hivyo, bastola hiyo ilipokonywa na kuangushwa chini na mwanachama mmoja
anayemuunga mkono Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad.
Wafuasi
wa chama hicho wanaomuunga mkono Maalim Seif waliumizwa kwa kupigwa na
wavamizi hao, huku waandishi wa habari licha ya kujitetea, lakini nao
waliambulia kipigo.
Waandishi
wa habari waliojeruhiwa ni Fred Mwanjala wa Channel Ten ambaye pia
aliharibiwa kamera yake, Merry Geofrey (Nipashe) aliyeumia sehemu ya
mkono na kushonwa nyuzi mbili, Rachel Chizoza (Clouds Fm), Kalunde Jamal
(Mwananchi), Henry Mwang’onde (The Guardian), Mariam Mziwanda (Uhuru),
Estherbella Malisa (Azam TV) na mwandishi wa habari hii Asha Bani wa
Gazeti la Mtanzania.
Baada
ya kundi hilo kuwapiga viongozi hao kwa takriban dakika 10, huku
wengine wakikimbia kujiokoa, ndipo wananchi waliokuwapo nje ya hoteli
hiyo walianza kurushia mawe magari mawili waliyokuja nayo.
Magari
hayo aina ya Prado yalipigwa mawe na kupasuka vioo vyote, huku mmoja
kati ya watu wa kundi hilo, akitajwa kwa jina moja la Kaduguda, alikatwa
kifundo cha mguu na kuachwa kikining’inia.
Mtu
huyo alianza kulia na kulalamika akiomba kuachiwa, huku akisema yeye
alibebwa bila ya kujua, huku akidai kuwa alitumwa na Mwenyekiti wa chama
hicho anayetambuliwa na ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa
Ibrahim Lipumba.
“Jamani nisameheni, mimi nimetumwa na Lipumba, naombeni mnisamehe jamani,” alilalamika huku akiendelea kulia.
Tukio
hilo lililokuwa kama filamu ya mapigano liliwashtua wananchi wa eneo
hilo waliokimbilia hotelini hapo, kila mmoja akisema lake, huku wengi
wao wakidhani kundi hilo lililovamia ni majambazi kutokana na magari
kukimbia na watu hao wakiwa wamejifunika sura zao.
Baadaye
saa 5:25, askari polisi wa Kituo cha Magomeni wakiongozwa na Inspekta
wa Polisi, Ahobokile Mwakabosi, walifika eneo la tukio na askari wengine
kwa gari mbili.
Gari
moja lilimchukua mtu aliyekatwa kifundo na kumpeleka Kituo cha Magomeni
na askari wengine walichukua maelezo kwa waliojeruhiwa, wakiwamo
waandishi wa habari.
Katika
hatua nyingine, uharibifu umefanyika katika hoteli hiyo, ikiwamo
kupasuka vioo, kuvunjwa kwa viti na kuumizwa kwa baadhi ya wafanyakazi,
akiwamo mlinzi wa getini.
Godfrey
Sombi aliyewahi kuwa mgombea udiwani wa Kata ya Mburahati, aliyeumizwa
kichwani, alisema jambo hilo si la kunyamaziwa kimya.
Alisema
vitendo vya uvamizi vimeendelea kutokea siku hadi siku kwa watu kutekwa
na kupelekwa kusikojulikana na wengine kujeruhiwa na kama Serikali
haitatoa tamko, kunaweza kusababisha mauaji yasiyo ya lazima.
Mlinzi
wa getini katika hoteli hiyo, Mandrit Luanda, alisema wavamizi hao
walifika wakiwa na magari yakiwa na bendera za CUF na hakuwa na wasiwasi
nao.
Alisema
waliingia licha ya kuanza kuwatilia shaka kutokana na kuwa na miili
mikubwa, lakini baada ya muda mfupi alianza kusikia mapigano yakiendelea
ndani ya hoteli hiyo.
“Baada
ya dakika 10 walitoka na kukimbia huku wenzao watatu wakijeruhiwa na
vioo vya magari waliyokuwa wamepanda vikivunjwa,” alisema.
MKUTANO
Awali
kabla ya mkutano huo kuvamiwa, Nkumbi, aliwaeleza waandishi wa habari
kuwa Mohamed Mkandu na Ally Makwilo wanajiita viongozi wa Wilaya ya
Ubungo ilhali wakijua wanafanya hivyo kinyume na katiba ya chama hicho.
Alisema
katika mkutano wao waliofanya Aprili 16, mwaka huu, walitoa matamko
makali kwamba ni marufuku kwa kiongozi yeyote kutofautiana na Lipumba na yeyote atakayefanya hivyo hatua kali zitachukuliwa dhidi yake.
Nkumbi
alisema kuwa hatambui uongozi wa muda wa Ubungo kwa kuwa hakuna kikao
chochote halali kilichotoa mwongozo wa uundwaji wa uongozi wa muda wa
wilaya hiyo mpya.
Aliwataka wanachama wa Kinondoni wasitoe ushirikiano wowote kwa hao viongozi aliowaita kuwa ni feki.
Pia
alisema anaunga mkono tamko lililotolewa na wanachama wa matawi 20 ya
Dar es Salaam la kumkataa Lipumba na kumtaka kuondoka katika ofisi Kuu
za Buguruni mara moja.
Aliwataka
wanachama wa chama hicho waliopo wilaya hiyo kuungana pamoja kuwakataa
Lipumba na lile aliloliita kuwa ni genge lake wanaotaka kuua chama na
upinzani kwa ujumla.
BAADA YA TUKIO
Taarifa
kutoka kwa Naibu Mkurugenzi wa Habari, Uenezi, Uhusiano na Umma wa CUF,
Mbarara Maharagande, ilisema wanalaani vikali kitendo hicho alichokiita
si cha kiungwana na hakiashirii nia njema, uvumilivu na uendeshaji wa
siasa za kistaarabu.
Alisema
kama Jumatano wiki hii, Katibu wa Wilaya ya Kinondoni, Mohamed Mkandu,
alifanya mkutano kama huo kwa amani bila bughudha na Watanzania
walisikia alichokizungumza, iweje Nkumbi afanyiwe vurugu hizo?
Kwa
niaba ya chama hicho, alitoa pole kwa waandishi wa habari waliojeruhiwa
katika tukio hilo na kwamba wataendelea kuwa nao pamoja katika
kuhakikisha kuwa wanarejea katika hali yao ya afya ili kutekeleza
majukumu ya kuwatumikia Watanzania.
“Tunalitaka
Jeshi la Polisi Mkoa wa Dar es Salaam kuwakamata wahusika wote wa tukio
hilo na kuwafikisha katika vyombo vya sheria kwa kuwa matukio kama haya
yanayofanywa na kundi linalojulikana yamekuwa yakijirudia mara kwa
mara, ikiwamo jaribio la utekaji kwa Kaimu Naibu Katibu Mkuu Tanzania
Bara, Joran Bashange mbali na wahusika wanne kukamatwa eneo la tukio,’’
alisema.
Maharagande alisema inasikitisha kuona polisi wamekalia mashtaka hayo na kushindwa kuchukua hatua za kisheria.
MATUKIO YALIYOWAHI KUTOKEA
Maharagande
alisema matukio kama hayo ni mwendelezo wa matukio mbalimbali
yaliyowahi kutokea na kusababisha vurugu zisizokuwa za lazima katika
mkutano Mkuu Maalumu wa CUF Taifa uliofanyika Agosti 21, mwaka jana.
Alisema
tukio la pili ni la utekaji wa wanachama na viongozi wa chama hicho
lililotokea Septemba 16, mwaka jana baada ya Bashange kutekwa akitoka
nyumbani kwake Mtaa wa Madenge, Buguruni, Wilaya ya Ilala na kupewa RB
namba BUG/IR/5937/2016.
Tukio
la tatu alisema lilitokea Ofisi Kuu ya chama hicho iliyopo Buguruni,
Dar es Salaam, Septemba 24, mwaka jana baada ya Lipumba na wafuasi wake
kuvamia ofisi hiyo, kuvunja mageti na milango ya ofisi, kuwapiga walinzi
binafsi wa Kampuni ya Ironsides Security Guard waliokuwa wakilinda hapo
na Jeshi la Polisi likatoa RB Na.BUG/RB/8741/2016.
Alilitaja
tukio la nne ni la uvamizi na kuvunja ofisi za Wilaya ya Bagamoyo na
Mkuranga lilitokea Novemba 4, mwaka jana na Lipumba na wafuasi wake
wakilindwa na polisi walikwenda katika ofisi hizo.
Alisema
tukio la tano ni la wabunge na wajumbe wa Baraza Kuu la Uongozi
kuzuiliwa kufanya mikutano na kukamatwa huko Nachingwea.
Alilitaja tukio la sita kuwa lilitokea Oktoba 10, mwaka jana baada mkutano kuzuiliwa kufanyika mkoani Tanga.
Na ASHA BANI – Mtanzania Dar es Salaam