8-1

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Mashaka Gambo amefanya uzzindua daraja la Mto Kijenge linalounganisha kata za Engutoto na Moshono ambalo limejengwa kwa ufadhili wa Kampuni ya Dharam Singh Hanspaul.

Akizungumza katika uzinduzi huo Mkuu wa Mkoa amesema daraja hilo ni ukombozi na msaada kwa wananchi wengi ambao walikua wakipata adha kubwa ya kuvuka haswa wakati wa mvua kutokana na kukosa kivuko cha uhakika na kivuko kilichokuwepo awali kiliashiria hali ya hatari kubwa kwa watoto, wazee, waendesha pikipiki, waenda kwa miguu wote na zaidi hakuna Gari lililokuwa na uwezo wa kupita hapo.
Hii ndio tunayoita kurudisha kwa jamii “Community Social Responsibility”, kampuni hii ya Hanspaul imetoa msaada ambao utatoa mchango mkubwa sana kwa jamii na sisi kama Serikali tunafarijika kwa kuona wadau wanaunga mkono jitihada za Serikaili kwa kiwango hiki hili ni jambo la kuigwa na Kampuni nyingine wajifunze katika hili.
Katika uzinduzi wa daraja hili Gambo alitumia fursa hiyo alisikiliza kero za wananchi waliohudhuria na ambao wamelalamikia uuzaji holela wa maeneo ya wazi ya Serikali hali inayopelekea uhaba wa maeneo ya kujenga huduma za kijamii kama zahanati na shule huduma ambazo hazipatikani katika kata ya Engutoto hiyo hivyo wameiomba serikali itatue tatizo hilo ili wananchi wapate huduma bora za ijamii.
Akiwasilisha kero zake mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Bi. Zaituni Marunda amesema kuwa licha ya uuzaji holela wa ardhi kuna migogoro ya ardhi katika kata hiyo na wananchi wengi  wanaomiliki ardhi bado hajapatiwa hati jambo ambalo linawapa wasiwasi kuwa huenda ardhi zao zikamegwa na wawekezaji.
Aidha Neema John aliongeza kuwa kwa kipindi kirefu katika maeneo hayo wamekuwa wakisumbuliwa na kero za maji, umeme na Zahanati hivyo wameiomba Serikali iwasaidie kutatua kero hizo znazowaathiri zaidi kinamama ambao hutembea umbali mrefu wakitafuta huduma za maji pamoja na kupata taabu wakati wa kujifungua.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mrisho Gambo ameagiza ofisi ya Mkurugenzi kumkabidhi ripoti ya maeneo ya wazi ya jiji yaliyouzwa kienyeji ili aweze kushughulikia kero na pia aliweza kuhamasisha ujenzi wa Zahanati ya Kata kwa kuchangia Bati 100 na kuungwa mkono na Bw. Hans Paul aliyetoa matofali 5000 huku Bw. Jagjit Aggarwal akichangia mifuko ya saruji 200 na Mkurugenzi wa Jiji Bw. Athumani Kihamia kuahudi kukamilisha ujenzi wa zahanati hiyo.
Daraja la Mto kijenge lilioanza kujengwa mwezi Juni na kukamilika Agost 2016 lina upana wa Mita 20, uwezo wa kupitisha magari yenye uzito wa Tani tatu(3), urefu kwenda juu ni mita 2.2, uimara wa pekee na linaweza kudumu kwa miaka 50; Ujenzi wake umegharimu kiasi cha shilingi milioni 67.

4-4Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe Mrisho Gambo(kwanza kulia) akipokea Kero kutoka kwa mwananchi kama zilivyowasilishwa na Mama Debora  wakati wa Unzinduzi wa Daraja la Mto Kijenge.
3-8Diwani wa Kata ya jirani ya Themi, Melance Kinabo akizungumza kuhusu changamoto zinazowakabili wakati wa uzinduzi wa Daraja la Mto Kijenge.
8-1Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo akizundua Daraja la Mto Kijenge.