WABUNGE WAISHAMBULIA SERIKALI, WAMRARUA WAZIRI WA FEDHA



Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu, akizungumza na wabunge wenzake baada ya kurudi bungeni akitoka kutumikia adhabu ya kutohudhuria mikutano miwili ya Bunge mjini Dodoma jana.


WABUNGE jana waliendelea kuchachamaa dhidi ya mawaziri na kusema kuwa Serikali ya Rais Dk. John Magufuli imekuwa na matumizi makubwa kuliko kile kinachopatikana, huku wakimtaja Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango kuwa ana kiburi na hashauriki.

Wakati wabunge mbalimbali wakiendelea kujadili Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa mwaka 2017/18 na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti, Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo), ameibua bomu jipya kuhusu matumizi ya Serikali kwa kipindi cha mwaka mmoja na kusema kuwa kuna tofauti ya Sh bilioni 78 za malipo ya mishahara ya watumishi katika kipindi cha mwaka mmoja.

Wakati Zitto akisema hayo, Mbunge wa Busega, Dk. Raphael Chegeni (CCM), alisema licha ya mipango ya maendeleo kupangwa na Bunge, lakini huenda ikakwama kutokana na kile alichokiita kiburi cha Waziri Dk. Mpango.

ZITTO

Zitto alisema kuwa pamoja na nia nzuri ya Serikali kubana matumizi, bado kuna ukakasi kwenye taarifa yake kuhusu matumizi ya fedha za mishahara kwa watumishi.

“Gharama za watumishi zinazotolewa kila mwezi na Waziri wa Utumishi na Utawala Bora, Angella Kairuki pamoja na zile za Benki Kuu (BoT) zinaonyesha kuanzia Agosti 2014 hadi Juni 2015 Serikali ililipa shilingi bilioni 456. Lakini pia ukiangalia taarifa za hadi Juni 2016 fedha zilizolipwa ni shilingi bilioni 534, tofauti ikiwa ni shilingi bilioni 18.

“Wakati Waziri Kairuki akisema katika taarifa zake kuwa wanaokoa shilingi bilioni 19 za watumishi hewa, ukichukua hesabu zote hizo kwa kipindi hiki utakuta Serikali imetumia zaidi ya shilingi bilioni 78. Sasa sijui nani mkweli kati ya waziri au BoT, hivyo kuna mmoja wao anadanganya umma, ni lazima utolewe ufafanuzi wa kina katika hili. Je, inakuwaje matumizi yawe juu zaidi wakati hakuna ajira mpya?” alisema Zitto na kuhoji.

Kuhusu sekta ya elimu ya juu nchini, mbunge huyo alisema ni jambo la kusikitisha kwa kipindi cha mwaka wa masomo 2017/18 wanafunzi waliokuwa na sifa za kupata mikopo ya Serikali ni 65,000 lakini waliopata ni 20,000 tu huku wengine wakikosa.

Zitto ambaye pia ni Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, aliponda hatua ya Serikali kutoa mkopo wa elimu ya juu kwa wanafunzi wanaosoma masomo ya sayansi tu na kuziacha fani nyingine.

Alisema nchi haiwezi kujengwa na wataalamu wa sayansi pekee, kwamba ni lazima Serikali iwe na utaratibu wa kufadhili masomo yote ya elimu ya juu ili wataalamu wa fani nyingine wapatikane pia.

“Huwezi kujenga uchumi wa viwanda kwa wanasayansi pekee. Je, hivi utakuwa na kiwanda kwa wanasayansi pekee bila kuwa na watu wa HR (wataalamu wa rasilimali watu), wahasibu na fani nyingine.

“Ili tuweze kufika huku, tuwe na utaratibu wa kutoa na ‘scholarship’ kwenye fani mbalimbali, na hili suala tulilijadili kwenye kamati kutwa nzima na Waziri Ndalichako (Profesa Joyce) alikuwepo,” alisema.

Zitto alisema anashangazwa na hatua ya Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Mpango kushindwa kusimamia andiko lake lililochapishwa katika jarida la Repoa, kuhusu hali ya umaskini, ikiwamo kile alichoshauri kuhusu uongozi na timu ya ushindi.

“Ili kulitekeleza hilo, ni lazima tuwe pamoja. Lakini sasa Serikali na Bunge hawako pamoja katika mikakati ya uendelezaji nchi. Serikalini mawaziri hawaelewani, ndiyo maana kila kukicha utasikia matamko na kutengeneza front pages (kurasa za mbele) za magazeti. Wabunge na Serikali tujichanganye maana sijui wapi tunakwenda,” alisema.

CHEGENI

Kwa upande wake, Mbunge wa Busega, Dk. Chegeni, alisema pamoja na utalaamu alionao Waziri Dk. Mpango, lakini ili afanikiwe lazima aondoe kile alichokiita kiburi.

“Chukua mawazo ya wabunge fanyia kazi, haiwezekani tupange mipango kwenye kitabu, lakini utekelezaji wake hatuambiwi iliyopita ikoje na wapi tumekwama.

“Ninajua Rais Magufuli ana nia njema na Watanzania, haiwezekani mawaziri kuwa na lugha tofauti. Kupitia mpango huu fanyia kazi hali ya uchumi, mzunguko wa fedha haupo mitaani na pia hata masilahi yetu wabunge yabebe.

“Rais anafanya juhudi kubwa ili Watanzania wanufaike na rasilimali zao, nanyi (mawaziri) msaaidieni, acheni kusigana,” alisema.

HECHE

Naye Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche (Chadema), alisema kuwa uchumi wa nchi hauwezi kwenda kwa maneno kwani anaona baada ya kutumbuliwa kwa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga atakayefuata ni Dk. Mpango.

Heche alisema nchi haiwezi kwenda bila kuwekeza kwenye elimu, lakini kinachofanywa sasa na Serikali ni kuwatesa wanafunzi wa elimu ya juu.

Alisema anashangazwa na mawaziri wa Serikali ya awamu ya tano kutoa kauli za kuwataka vijana wakajiajiri, huku wao ambao wengine ni maprofesa, madaktari na hata wanasiasa wa kawaida wamekimbilia kuomba ajira za wananchi.

“Ninashangaa sana kila siku mnasema vijana mjiajiri, watajiajiri vipi? Na kama nyepesi mbona wewe umekimbilia huku? Tena wengine ni maprofesa na madaktari. Tena na mama Ndalichako (Joyce) nilikuwa na kuheshimu kweli ulipokuwa pale Baraza la Taifa la Mitihani (NECTA) ukionyesha wanafunzi waliochora zombie, lakini leo wewe ndiyo umechora zombi kubwa ambalo halijapata kutokea.

“Kuna mwingine mnamwita ‘Mzee wa Sound’, ukimsalimia anaweka mikono mifukoni anakuuliza unataka kiwanda? Sijui hicho kiwanda amekiweka mfukoni,” alisema Heche.
 Na Bakari Kimwanga-Mtanzania DODOMA
Powered by Blogger.