20160308211407

Licha ya juhuhudi ambazo zimekuwa zikifanywa na serikali la kupunguza ajali, takwimu zinaonyesha ajali za barabarani zimeongezeka kwa asilimia 42 kuanzia mwezi Januari hadi Septemba, 2016 ambapo takwimu zinaonyesha jumla ya ajali 4,442 zilitokea katika kipindi hicho kulinganisha na ajali 2,561 zilizotikea kipindi kama hicho mwaka jana.

Takwimu hizo zimetolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama Barabarani Mkoa wa Dar es Salaam, Elifadhili Mgonja wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu Maadhimisho ya Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani.
Mgonja amesema pia katika kipindi hicho ajali za majeruhi ziliongezeka kwa asilimia 22 ambapo takribani watu 3,127 walijeruhiwa ukilinganisha na watu 2,438 waliojeruhiwa kuanzia Januari hadi Septemba, 2015.
Hata hivyo, amesema kuna upungufu wa ajali za vifo kwa asilimia 6 ambapo kuanzia Januari hadi Septemba, 2016 zilitokea ajali 216 ambayo ni idadi pungufu ya 14 ya ajali zilizotokea kipindi kama hicho mwaka 2015.
Kuhusu maadhimisho ya nenda kwa usalama, amesema mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda.
Amesema maadhimisho hayo yatafanyika katika viwanja vya MwembeYanga, Temeke kuanzia Novemba 7 hadi 11, 2016.
Amesema maadhimisho hayo yataambatana na ukaguzi wa vyombo vya moto vya usafiri vikiwemo pikipiki, daladala na magari, utolewaji wa elimu ya usalama barabarani hususani kwa madereva bodaboda kutokana kwamba ndiyo chanzo cha ajali za barabarani.