Wahariri waukubali Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari
Wahariri
wa vyombo vya habari wameukubali Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari
baada ya kuusoma kwa umakini nakuona namna gani utasaidia kuinua tasnia
ya habari nchini.
Hayo
yamebainishwa katika mahojiano maalum kwa njia ya simu na baadhi ya
wahariri wa vyombo vya habari akiwemo Mhariri wa Televisheni ya TV 1,
Bw.Said Mwishehe huku akieleza faida za Muswada huo pamoja na kutoa
maoni yake kwa kuiomba serikali kuangalia vizuri baadhi ya vipengele na
kama kipengele cha 54 na 55 katika Sehemu ya Nane ili kuvipunguzia
makali na kuondoa suala la kuonekana kubana uhuru wa vyombo vya habari.
“Kuna
umuhimu kwa wadau wa habari kuunga mkono muswada huu badala ya kuupinga
kwani una mambo mazuri yatakayosaidia kuboresha tasnia hii ya habari na
kuipa heshima kama taaluma nyingine badala ya kuonekana kuwa waandishi
wa habari ni watu wababaishaji tu na wasiyo na taaluma iliyo
imara,”alisema Bw.Mwishehe.
Pamoja na
hayo Mhariri huyo aliendelea kusema amefurahishwa na muswada kwa namna
unavyojali maslahi ya waandishi wa habari pale unapoeleza kuwa wamiliki
wa vyombo vya habari watahitajika kuwakatia bima waandishi wa habari kwa
hiyo itakuwa jambo la busara kwani waandishi wamekuwa wakifanya kazi
katika mazingira magumu yanayohatarisha afya zao pasipo kuwa na bima
inayomlinda akiwa kazini.
Aidha,
Bw.Mwishehe aliwasihi wadau wa sekta ya habari kutuma maoni yao kwa vile
vipengele vya muswada vinavyoonyesha kutokuwa sawa na pia ameiomba
serikali kuwa na utayari wa kuyapokea maoni hayo kwa ajjili ya kuboresha
muswada huo na kuufanya bora na wenye tija katika tasnia ya habari
nchini.
Naye
Mhariri wa Gazeti la Mtanzania, Bw.Revocatus Makaranga alisema Muswada
huo wa habari una mambo mazuri yanayoipeleka tasnia mahali pazuri
ikiwemo suala la waandishi wa habari kuhitajika kujiendeleza katika
elimu ya juu na hii itasaidia kukuza upeo wa mwandishi na kumfanya awe
na uwezo mkubwa na kufanya kazi kwa kujiamini kama ilivyo kwa waandishi
wa nchi zilizoendelea.
Bw.Makaranga
aliongeza kusema muswada una vipengele ambavyo ipo haja ya serikali
kuvifanyia marekebisho ikiwemo suala la adhabu inayotolewa kwa waandishi
ya kuwafungia pale wanapokuwa wamekosea.
Pia
mhariri huyo ameipongeza serikali kwa muswada huo ambao utaleta picha
mpya ya kimaendeleo katika tasnia ya habari ikiwemo suala la kuanzishwa
kwa Mfuko wa mafunzo kwa wanahabari nchini ambapo utasaidia kutoa elimu
kwa waandishi mara kwa mara na kuwajengea uwezo wa utendaji.
Kwa
upande wake, Mhariri Mkuu wa kituo cha Redio Efm, Bi Scolastika Mazula
alisema katika muswada huo wa habari yapo mambo mazuri yenye tija katika
sekta ya habari kama suala la kuanzishwa kwa Mfuko wa mafunzo kwa
wanahabari ni jambo jema sana kwani utasaidia kutoa fursa za waandishi
kujiendeleza kimasomo na kuifanya fani ya habari kuwa na wasomi zaidi
tofauti na inavyoonekana kwa sasa.
“Suala la
elimu kwa waandishi ni bora liwekwe wazi kisheria kwani tansnia hii ya
habari inahitajika kuheshimika kama ilivyo tansia nyingine badala ya
kuonekana wababaishaji”, alisema Mazula.
Pamoja na
hayo Bi. Mazula aliendelea kutoa maoni yake kuhusu Muswada kwa kusema
kuwa suala la kuanzishwa kwa bodi ni zuri ila ingekuwa vyema kama bodi
hiyo itakuwa na asilimia kubwa ya wadau wa habari na ijitegemee na
Waziri mwenye dhamana ya habari na Mwanasheria Mkuu wasiwe na mamlaka
sana katika bodi hiyo.
Pamoja na
hayo naye Katibu wa Jukwaa la Wahariri, Bw.Neville Meena alisema kwa
sasa wanajukwaa wameshatoa maoni yao kuhusu muswada huo na
watayawasilisha kwa ajili ya kusaidia kuboresha muswada huo na kuufanya
uwe na tija na manufaa zaidi katika kuendeleza tasnia ya habari nchini.(P.T)