Dk. Charles Msonde

 Baraza la Mtihani Tanzania (NECTA) limetangaza matokeo ya mtihani wa Taifa wa Darasa la saba uliofanyika Septemba 8 hadi 9, 2016 Tanzania Bara, limesema kuna baadhi ya shule zilifanya udanganyifu kwa kuiba mitihani, kuandaa majibu na kuwapa watahiniwa jambo ambalo ni kinyume cha kanuni za mitihani.

Katibu Mtendaji wa NECTA, Dk. Charles Msonde leo amewaambia waandishi wa habari kuwa takribani shule 6 zimefanya udanganyifu huo.
Amesema baraza hilo limeshatoa taarifa za waliohusika na kushiriki udanganyifu wa matokeo kwa mamlaka zao za utumishi ili wachukuliwe hatua kwa mujibu wa kanuni za utumishi wa umma.
“Pamoja na kazi nzuri iliyofanywa na waendeshaji wa mitihani hiyo, kulijitokeza matukio machache ya udanganyifu yaliyofanywa na baadhi ya wasimamizi wa mitihani, wamiliki wa shule na walimu wakuu,” amesema.
Amezitaja shule zilizofanya udanganyifu kuwa ni pamoja na Tumaini iliyopo Sengerema mkoani Mwanza ambapo mmiliki wake Jafari Mahunde anatuhumiwa kuiba mtihani, kuandaa majibu ambayo watahiniwa waliyaandika kwenye sare za shule na kuyatumia ndani ya chumba cha mtihani.
Shule nyingine ni ya Little Flower iliyopo Serengeti mkoani mara ambapo mwalimu mkuu wa shule huyo Cecilia Nyamoronga anadaiwa kuiba mtihani na kuandaa majibu na kumpa msimamizi mkuu pamoja na wasimamizi ili wawapatie watahiniwa.
Shule nyingine alizozitaja ni Mihamakumi iliyopo Sikonge,Tabora, Qash iliyopp Babati mkoani Manyara, St. Getrude Madaba mkoani Ruvuma, na Kondi Kasandalala iliyopo Sikonge mkoani Tabora.
Jumla ya shule 16,350 zilishiriki katika mtihano huo, ambapo watahiniwa 795,739 walisajiliwa kufanya mtihani huo.