makondaaa

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda leo ametoa agizo kwa wafanyabiasara ndogondogo (wamachinga) wanaofanya biashara pembezoni mwa barabara kuondoka na kwenda katika maeneo rasmi waliyopangiwa kufanya shughuli zao.

Makonda ametoa agizo hilo leo wakati akizungumza na waandishi wa habari, ambapo amesema kuwa, ongezeko la wamachinga barabarani limesababisha serikali kupoteza mapato zaidi ya bilioni 100 kwa mwezi uliopita na kwamba Halmashauri ya Manispaa ya Ilala imepoteza mapato zaidi ya milioni 50.
Makonda amesema kuwa, kurudi kwa wamachinga hao pia kumesababisha ongezeko la matukio ya uporaji, sambamba na kuhatarisha usalama wa watumiaji barabara hizo hasa zile za mabasi yaendayo mwendo wa haraka (DART).
“Wananchi baadhi wanalalamika kuwa matukio ya uporaji yameongezeka, na pia usalama umepungua katika maeneo husika,” amesema.
Ameongeza kuwa “Natoa wito kwa wamachinga waondoke barabarani, hatukuweka rami kwa ajili ya wao kufanya biashara, bali zitumiwe na waenda kwa miguu, waendesha vyombo vya moto, tunajua kuwa wanatafuta ridhiki za familia zao ila wafuate sheria na taratibu za nchi”
Makonda amewataka wakurugenzi wa Halmashauri za wilaya zilizopo jijini Dar es Salaam ndani ya siku 14 wawe wameshatenga maeneo rasmi ya wafanyabishara ndogondogo ambao hawakupata maeneo.
Hali kadhalika ametoa wito kwa wamachinga wasio na maeneo rasmi ya kufanya biashara, kwenda katika halmashauri husika ili wapangiwe maeneo ya kufanyabiashara. Pia ametoa agizo kwa wamiliki wa nyumba kutoruhusu wafanyabiashara kupanga bidhaa zao mbele ya nyumba kwa kuwa kitendo hicho huikosesha serikali mapato.
“Wenyenyumba ambao wanahifadhi wafanyabiashara watueleze kama wanapewa kodi wanazipelela wapi?, masoko yako wazi hayana wafanyabiashara na kusababisha manispaa kukosa kodi,” amesema.