MWANZA, ARUSHA WANG’ARA MBIO ZA BAISKELI SIMIYU.;
Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Tulia Ackson (mwenye baiskeli wa pili kulia) akiwa na viongozi wa Mkoa na baadhi ya Wabunge wa Mkoa wa Simiyu na Viti Maalum kutoka nje ya Mkoa kwa ajili ya kufungua mashindano ya baiskeli yaliyofanyika Mjini Bariadi.
Mshindi wa kwanza wa mbio za baiskeli kilometa 200 kwa wanaume, Hamisi Hussein kutoka Arusha akipanda kwenye pikipiki yake aliyokabidhiwa baada ya kuibuka mshindi dhidi ya wenzake katika mashindano ya Baiskeli yaliyofanyika Mjini Bariadi Mkoani Simiyu.Add ca
Mshindi wa tatu mbio za baiskeli kilometa 80 (wanawake), Vumilia Mwinakila kutoka Mkoa wa Simiyu akicheza wimbo wa Kisukuma pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka na Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Tulia Ackson baada ya kupokea kitita cha shilingi laki tatu.
Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Tulia Ackson (wa pili kushoto) akimkabidhi ufunguo wa pikipiki mshindi wa kwanza kilometa 200 (wanaume), Hamisi Hussein kutoka Arusha katika mashindano ya Baiskeli yaliyofanyika Mjini Bariadi (kulia) ni Mkurugenzi Kampuni ya Jambo Food Products ambayo ni mdhamini, Mhe.Salum Khamis akimpongeza Mshindi huyo.
Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Tulia Ackson akimkabidhi ufunguo wa pikipiki mshindi wa kwanza (wanaume) katika mashindano ya Baiskeli yaliyofanyika Mjini Bariadi kilometa 200, Hamisi Hussein kutoka Arusha.
Washiriki wa mashindano ya mbio za Baiskeli kilometa 200 wanaume (kulia) wakiendelea kuchuana vikali kushindania pikipiki na fedha taslimu.
Na MAKALIBLOG, SIMIYU;
Hatimaye Mashindano ya mbio za Baiskeli, yaliyohusisha washiriki kutoka mikoa ya Mwanza, Simiyu na Arusha yamekamilika mkoani Simiyu, ambapo mshindi kwa upande wa wanaume akitokea Mkoa wa Arusha na mshindi upande wa wanawake akitokea jijini Mwanza.
Mashindano hayo ambayo yalidhaminiwa na kampuni ya vinywaji vya Jambo Food Product kwa mara ya kwanza yameandika historia kwa Mkoa wa Simiyu yalimalizika , huku idadi kubwa ya watu wakijitokeza kushuhudia mbio hizo za baiskeli ambazo zilianzia eneo la Salunda na kumalizikia katika viwanja vya Halmashuri ya Mji wa Bariadi umbali wa km 200 kwa wananume na km 80 kwa wanawake.
Akizungumza katika mashindano hao, Naibu Spika wa Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Tulia Ackson ambaye alikuwa mgeni rasmi wa mbio hizo kwa mwaka 2017, amesema Mkoa wa Simiyu umeandika historia na kwamba mikoa mingine ijufunze kutoka Simiyu, huku akitoa wito kwa wanawake kushiriki kwa wingi kwenye michezo.
Tulia alisema kuwa michezo nchini haijapewa kipaumbele lakini ikitumiwa vizuri inaweza kutoa ajira ukiwemo mchezo wa mbio za baiskeli; ambapo ametoa wito kwa viongozi wa mikoa mingine pia kuwekeza katika michezo mbalimbali ili kuwasaidia wananchi kupata kipato.
“Lililofanyika Simiyu ni jambo jema sasa hivi watu watakuwa wanajua kuwa wakijifua vizuri kwenye baiskeli na ngoma za jadi wanakuja kushiriki mashindano ya Baiskeli na ngoma Simiyu, nitoe wito kwa viongozi wengine kufikiria mambo mengine yanayoweza kuwasaidia wananchi katika maeneo yao kupata ajira na kujipatia kipato” alisema.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka amesema mkakati wa mkoa huo ni kurasimisha tamaduni zote na kuhusianisha na shughuli za Utalii ndani ya mkoa huo.
“Position(Nafasi) ya Mkoa wa Simiyu kwenye nchi ni kukuza tamaduni na sanaa zetu kama moja ya eneo litakalotuunganisha na sekta ya Utalii, tumezungukwa na mapori ya akiba na mbuga za wanyama, tungehitaji watalii wanapokuja kwenye maeneo hayo wapate ladha ya tofauti kiwemo utamaduni wa Mtanzania”
Mtaka aliongeza kuwa wasanii wote watatambuliwa na baadae kujengewa uwezo kupitia watalaam wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam(Kitivo cha sanaa),Chuo cha Sanaa Bagamoyo na vyuo vya michezo ili waweze kufanya kazi zao kibiashara na kuimarisha uchumi wao.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kampuni ya Jambo Food Products,Mhe.Salum Khamis ambaye ndio Mdhamini wa mashindano ya Baiskeli na ngoma za Asili (Simiyu Jambo Festival) amesema ataendelea kudhamini mashindano kama hayo Mkoani Simiyu ili kuwawezesha wananchi kuinua kipato kupitia vipaji vyao.
Mshindi wa kwanza mbio za kilometa 80 (wanawake) Raulensia Luzuba kutoka Mwanza ameomba mashirika na makampuni mbalimbali kuwadhamini ili waweze kujengewa uwezo na kuandaliwa kushiriki katika mashindano ya Kimataifa.
Masunga Duba mshindi wa mbio za kilometa 200(wanaume)kutoka Simiyu amesema pamoja na wafadhili kudhamini mashindano wawasaidie pia wachezaji kupata baiskeli za kisasa zitakazowasaidia kwenda kwa kasi inayotakiwa.
Mashindano ya baiskeli Mkoani Simiyu yameshirikisha wachezaji kutoka mikoa ya Simiyu, Mwanza, Shinyanga,Arusha na Mbeya, ambapo ushindi kwa upande wa wanaume umechukuliwa na Hamisi Hussein(Arusha) ambaye amejishindia pikipiki, wa pili ni Masunga Duba(Simiyu) kitita cha shilingi 1,000,000/= wa tatu Richard Laizer(Arusha) .shilingi 500,000/= na zawadi nyingine zimetolewa kwa mshindi wa nne mpaka wa 15.
Kwa upande wa wanawake mshindi wa kwanza Raulensia Luzuba kutoka Mwanza amejipatia shilingi 500,000/=, mshindi wa pili Tatu Malulu(Mwanza) shilingi 400,000/= na wa tatu ni Vumilia Mwinamila(Simiyu) shilingi 300,000/= na zawadi nyingine zimetolewa kwa mshindi wa nne mpaka wa 10.
Walemavu mshindi wa kwanza Emmanuel Mtemi amejipatia shilingi 200,000/= wa pili Masunga Sendama shilingi 150,000/= na wa tatu Saguda Sospeter shilingi 100,000/=wote kutoka mkoa wa Simiyu na zawadi nyingine zimetolewa kwa mshindi wa nne na wa tano.