MTUMISHI WA UMMA ATAKAYESHINDWA KUWASILISHA CHETI AU INDEX NUMBER ATAKUWA AMEJIONDOA KAZINI MWENYEWE
MTUMISHI wa umma atakayeshindwa
kuwasilisha cheti cha elimu na taaluma au “Index number” ya mtihani ili
zihakikiwe na Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), itakapofika Machi
mosi mwaka huu, atakuwa kajiondoa kazini mwenyewe, imeelezwa.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais
(Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora), Angellah Kairuki
alibainisha hayo mwishoni mwa wiki wakati akifungua Mkutano wa Watendaji
Wakuu wa Wakala za Serikali jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.
“Watendaji wakuu ninawaomba msimamie
uhakiki wa vyeti ili watumishi wenu wafanye kazi kwa sifa stahiki,”
alisisitiza Kairuki, katika taarifa iliyotolewa na wizara yake.
Aliongeza kwamba serikali ilisitisha
ajira mpya ili kupisha kazi ya kuondoa watumishi hewa, ambayo imefika
ukingoni na siku za karibuni, ajira zitarudishwa.
Akiwa mjini Dodoma, Septemba mwaka jana,
wakati wa kuapishwa kwa wakurugenzi watendaji wapya 13 walioteuliwa
Septemba 10, mwaka huu, Kairuki alisema kuanzia serikali imewaondoa
watumishi hewa 17,201 kwenye utumishi wa umma na kazi hiyo inaendelea.
Kairuki aliwataka watendaji wakuu kuweka
mikakati ya kuepuka watumishi hewa na kusimamia kwa dhati kwa sababu
jambo hilo, limeumiza na kupoteza rasilimalifedha nyingi za serikali.
Alisema anatambua kuna wakala zenye
upungufu wa watumishi, hivyo zinaingia gharama kubwa za kuajiri
wafanyakazi wa mikataba, hata hivyo alielekeza kila Mtendaji Mkuu
ajiridhishe kwa kuandaa taarifa ya mahitaji halisi ya watumishi.
Pamoja na hilo, Kairuki alielekeza
wakala zenye watumishi wa mikataba zifanye tathmini na kuhakiki kama
kweli watumishi hao wanahitajika kwa kuwa eneo hilo ni moja ya maeneo
yenye ajira za mashaka kwa baadhi ya taasisi.
Aliongeza kuwa yapo malalamiko kuhusu suala la maadili na uwajibikaji yanayozigusa Wakala za Serikali.
Aliainisha masuala hayo ni pamoja na
watumishi hewa, taarifa chafu za watumishi, matumizi mabaya ya madaraka
na rasilimali za umma, kutosimamia ipasavyo utekelezaji wa mifumo ya
utendaji kazi na wakati mwingine kutotekeleza majukumu ya msingi ya
wakala.
Alifafanua kuwa amegundua kupitia
taarifa mbalimbali kuwepo kwa changamoto ya mawasiliano hafifu kati ya
wizara mama na wakala zilizo chini yao ambapo taarifa kutoka katika
wakala hazichambuliwi inavyostahili na hata zinapochambuliwa na wizara
mama, hazitoa mrejesho kwenda katika wakala.
Awali, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais
(Utumishi), Dk Laurean Ndumbaro alizitaka wakala za serikali kuimarisha
eneo la ufuatiliaji na tathmini ili kuimarisha utendaji kazi na kuleta
mabadiliko yanayotarajiwa na Watanzania.